Waasi wa M23 waendelea kuajiri vijana wapiganaji mjini Goma
30 Aprili 2025Timu ya kuhamasisha na kusajili vijana ya muungano wa waasi wa AFC na M23 imetajwa kuendesha zoezi hilo katika mitaa ya Murara mjini Goma. Innocent Munyemana ambaye ni miongoni mwa wakuu wa timu hiyo amefahamisha kuwa wanawahimiza vijana kujiunga na kile wanachokiita jeshi la mapinduzi la Kongo.
"Tumetoa mwito kwa vijana ambao wangependa kujiunga na jeshi la mapinduzi la Congo wafanye hivyo kwani ni jeshi linalozingatia utaalamu, limeelimika na kujitolea kupambana na utawala duni na mienendo mingine mibaya", alisema Menyemana.
Umoja wa Mataifa washutumu uajiri wa kulazimishwa
Kijana aliyejitambulisha kwa jina la Salomon kutoka mtaa huo amelezea kwa nini ameamua kujinga na uasi
"Nimeamua kwa hiari kujiunga na M23 kwa sababu nimeshawishika kwamba vuguvugu hilo linapigania maendeleo. Ninajitenga na utawala wa aliyekuwa gavana wa Tshilombo ambaye alitoa ahadi ambazo hakuzitimiza. ndiyo maana kwa hiari yangu nimeamua kujiunga na M23", aliiambia DW.
Zoezi hili la kuwasajili vijana kuwa wapiganaji linaendelea katika maeneo mbalimbali hata katika mkoa wa Kivu Kusini. Katika ripoti yake ya hivi karibuni Umoja Mataifa imefahamisha kuwa zoezi hilo limekuwa likifanyika huku baadhi ya vijana na watoto wakilazimishwa kujiunga tangu mwezi Aprili mwaka 2024.
Waasi wa M23 wakaidi miito ya kuondoka Goma
Maelfu ya vijana na watoto hao wamepitia mafunzo katika miezi michache iliyopita. Kulingana na mdadisi mmoja Moise Hangi, lengo la waasi hao ni kuwa na nguvu za ushawishi kwenye meza ya mazungumzo kutokana na idadi kubwa hata kama wataondoka maeneo waliyoyateka.
"Hii leo katika mitaa ya mji isiyo na uthabiti, vijana wanasajiliwa kujiunga na uasi. Bila shaka, waasi wanajiimarisha kwa idadi ili wadai kwamba askari wao wajumuishwe katika jeshi la taifa la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baada ya mazungumzo yaliyoanzishwa Doha na Washington. Tunaamini serikali ya Congo inatakiwa kubaki kuwa chonjo sana.",
Miito ya kuwataka waasi wa M23, wanaodaiw akuungwa mkono na jeshi la Rwanda, kuondoka maeneo waliyoyateka ya mashariki mwa Kongo imendelea kuongezeka. Lakini hali halisi katika uwanja wa mapambano ni kwamba hakuna dalili ya hilo kufanyika.