Waasi wa Houthi wavamia ofisi za UN, wateka wafanyakazi
1 Septemba 2025Waasi wa Houthi wamevamia ofisi za mashirika mawili ya misaada ya Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa, na kuwateka nyara wafanyakazi kadhaa.
Taarifa hizo ni kwa mujibu wa shirika la habari la dpa likinukuu vyanzo vya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen jana Jumapili.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, waasi hao walivamia ofisi za shirika la Mpango wa Chakula Duniani WFP na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF, na kuwateka takriban wafanyikazi 10 ambao walichukuliwa na kupelekwa sehemu isiyojulikana. Sababu za kutekwa kwao bado hazijajulikana.
Waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran, ambao wamekuwa wakidhibiti mji wa Sanaa na maeneo makubwa ya kaskazini mwa Yemen kwa karibu muongo mmoja, bado hawajatoa tamko lolote rasmi kuhusu tukio hilo.
Katika taarifa aliyoitoa jana, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen, Hans Grundgerg, amelaani wimbi jipya la utekaji wa wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa pamoja na uvamizi wa ofisi zao na kunyakuliwa kwa mali zao.