Wahouthi wakiri kuishambulia meli ya Kigiriki
7 Julai 2025Meli hiyo sasa imezama katika Bahari ya Shamu baada ya kushambuliwa kwa kutumia boti ndogo zilizojaa mabomu na makombora. Wafanyakazi wake 22 waliokolewa baada ya kuitelekeza meli hiyo inayoitwa Magic Seas.
Maafisa wa ulinzi wa meli wa Uingerezawamesema shambulizi hilo lilitokea Jumapili,na kwamba meli hiyo ilivamiwa kwa risasi na mabomu ya kurushwa kwa roketi kabla ya kushambuliwa na mabomu ya mitumbwi ya kasi. Kampuni ya usalama ya Ambrey imethibitisha kuwa boti mbili zilizojaa mabomu ziliigonga meli hiyo, huku nyingine mbili zikiharibiwa na walinzi waliokuwa ndani ya meli.
Kulengwa kwa bandari ya Hodeida
Hali hii iliichochea Israel kufanya mashambulizi ya anga mapema Jumatatu yaliyolenga bandari na miundombinu inayodhibitiwa na waasi wa Kihouthi huko Hodeida, Ras Isa na Salif. Jeshi la Israel limedai kuwa bandari hizo zinatumiwa na Wahouthi kupokea silaha kutoka Iran kwa ajili ya mashambulizi dhidi ya Israel. Msemaji wa kijeshi wa Wahouthi, Brigedia Jenerali Yahya Saree, amedai kuwa vikosi vyao vya anga "vilifanikiwa kuzikabili” ndege za Israeli, ingawa hakutoa ushahidi.
Wahouthi walijibu kwa shambulizi la makombora na droni, wakirusha makombora 11 kuelekea Israel. Saree amesema hatua hiyo ilikuwa ni jibu kwa "uchokozi wa Israel” na kuonesha mshikamano na watu wa Palestina. Zaidi Jenerali Saree anasema "Tuko tayari kwa mapambano ya muda mrefu, kukabiliana na majaribio ya kuvunja mzingiro wa baharini uliowekwa na vikosi vyetu dhidi ya adui, katika kuwaunga mkono watu wetu wa Gaza."
Kushindwa kwa Jeshi la Israel kuyazuia makombora ya Houthi
Jeshi la Israel lilisema kuwa lilijaribu kuyazuia makombora hayo ya Wahouthi, lakini yakionekana kufika malengo yao, ingawa hakuna ripoti za majeruhi hadi sasa. Hili linajiri wakati Israel inazidi kufanya mashambulizi peke yake dhidi ya waasi hao, tofauti na awali waliposhirikiana na Marekani. Mnamo Aprili, Marekani ilishambulia bandari hizo na kuua watu 74, lakini kwa sasa Israel imechukua jukumu hilo pekee.
Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alisema Israel haitavumilia mashambulizi yoyote na kuonya kuwa Wahouthi wataendelea kubeba gharama kubwa kwa vitendo vyao. Shambulizi dhidi ya meli ya Magic Seas lilitokea kilomita 100 kusini magharibi mwa Hodeida, katika eneo linalodhibitiwa na Wahouthi. Meli hiyo ilikuwa njiani kuelekea Mfereji wa Suez nchini Misri. Ujumbe wa kijeshi wa Umoja wa Ulaya, Operation Atalanta, ulisema kuwa mabaharia 22 walikuwa ndani ya meli hiyo. Wote waliokolewa salama na meli nyingine iliyokuwa ikipita karibu.
Madai ya Iran kuendelea kuwapa Wahouthi Silaha
Waziri wa Habari wa serikali ya Yemen inayopambana na Wahouthi, Moammar al-Eryani, ameshtumu shambulizi hilo na kusema linaonesha wazi kuwa Wahouthi ni chombo cha Iran chenye lengo la kuvuruga utulivu wa kikanda na kimataifa. Amesema Iran inaendelea kuwapa Wahouthi silaha, makombora, droni na mabomu ya baharini.
Takwimu zinaonyeha kuwa kati ya Novemba 2023 na Januari 2025, Wahouthi walishambulia zaidi ya meli 100 za kibiashara, wakazamisha mbili na kuua mabaharia wanne. Licha ya kushuka kwa shughuli za usafirishaji katika Bahari ya shamu, hali imeanza kurejea taratibu katika wiki za karibuni.
Mashambulizi haya yanajiri wakati hali ya Mashariki ya Kati inazidi kuwa tete, huku mchakato wa amani kati ya Israel na Hamas ukiwa katika hatihati, na Iran nayo ikitathmini iwapo itarejea kwenye mazungumzo kuhusu mpango wake wa nyuklia baada ya kushambuliwa na Marekani. Waangalizi wanaonya kuwa mgogoro huu unaweza kuvuruga zaidi biashara ya kimataifa na kuibua mashambulizi mapya ya kisasi.