Waasi wa M23 wauteka mji wa Walikale licha ya mwito wa amani
20 Machi 2025Taarifa kutoka Walikale zinasema waasi wa M23 waliuteka mji huo Jumatano jioni baada ya milio ya risasi ya hapa na pale. Mmoja ya viongozi wa jadi wa mji wa Walikale amesema waasi hao walipenyeza ngome ya jeshi na kutumia njia mbadala kuufikia mji huo.
Mji wa Walikale ni watatu kwa uzalishaji wa madaini ya bati ulimwenguni. Na umekuwa mji wa kimkakati ambao unaunganisha majimbo manne ya mashariki mwa Kongo yakiwemo : Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Tshopo na Maniema.
Mji wa Walikale wenye wakaazi wapatao 15,000 ni umbali wa kilomita 125 na mji wa Goma na chini ya Kilomita 400 na Kisangani. Umoja wa Mataifa umesema kwa wiki kadhaa sasa zaidi ya watu laki moja wamekimbia maeneo hayo na kuelekea mji wa Lubutu mkoani Maniema.
Mapigano yanaendelea huko Kivu, licha ya mwito wa usitishaji mapigano wa haraka na usio na masharti, uliotolewa Jumanne na marais Felix Tshisekedi na Paul Kagame baada ya mkutano wao wa ana kwa ana wa mjini Doha, Qatar.
Macron aunga mkono juhudi za amani Kongo
Mwito huo umeungwa mkono na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ambaye alikutana pia viongozi wa kidini wa Kongo mjini Paris hapo Jumatano.
Baada ya mazungumzo yao na Macron, Askofu Fulgence Muteba, mwenye kiti wa Kongamano la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Kongo, CENCO amesema mpango wa amani wa viongozi wa kidini unalenga kuwaweka pamoja si tu serikali na waasi wa M23 bali wanasiasa wote na mashirika ya kiraia ilikutafuta suluhisho la kudumu la mzozo wa Kongo.
"Ni wiki kadhaa sasa ambayo tumekuwa tukiomba kuweko na mazungumzo, kwa sasabu magigano hayawezi kuleta suluhisho kwa mzozo huu. Umwagaji damu unazua majonzi pekee, kwa hiyo kwetu sisi nilazima Wakongo wakee pamoja kwenye meza ya mazungumzo kwa ajili ya maelewano na mshikamano wa kitaifa na inaomba kila mmoja wetu aache majigambo", alisema Muteba.
Vibaraka wa Rwanda ?
Kwenye mahojiano hapo jana na gazeti la Ufaransa la Le Figaro, rais Tshisekedi amesema yuko tayari kwa mazungumzo zaidi ya moja kwa moja na Rais wa Rwanda Paul Kagame baada yale ya mjini Doha. Akisema kwamba upatanishi wa Qatar umefanyika kwa busara.
Hata hivyo Tshisekedi amekosoa vikali hatua ya waasi wa M23 ya kutohudhuria mazungumzo ya amani ya Luanda, nchini Angola. Akisema hiyo ni ishara tosha kwamba M23 ni vibaraka wa Rwanda na wamekuwa watiifu kwa kauli ya kiongozi wa Rwanda pekee.