Waandishi Habari wahatarisha maisha kuripoti mzozo wa Sudan
23 Aprili 2025Ugumu wa upatikanaji wa habari nchini Sudan unazidi huku wengi wakiwa tayari wameshaikimbia nchi huyo kunusuru maisha yao.
Mazingira ya usambazaji wa taarifa yanazidi kuwa magumu hali inayosababisha waandsihi kukimbilia milimani kutafuta huduma za mawasiliano ambazo zimezorota kwenye maeneo mengi ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, waandishi wa habari walioko Sudan wakiripoti habari za mapigano hayo sasa wanawindwa sio tu katika uwanja wa mapigano bali mpaka kwenye makaazi yao na huku baadhi ya vyombo vya habari vikifunga ofisi zao na kukimbilia nje ya Sudan.
Kuyumba huku kwa usalama wa waandishi wa habari kumesababisha wengi kufanya kazi kwa usiri ili kunusuru maisha yao kutoka na vitisho wanavyokutana navyo ili kuzuia taarifa juu ya mapigano hayo kufahamika.
"Hakuna anayeweza kujua ninachofanya na wakigundua watanikamata na wakinisamehe watachukua simu yangu pekee", amesema mmoja wa waandishi wa habari aliyeko eneo la mapigano wakati akihojiwa na shirika la habari la AFP.
Waandishi wahamisha makaazi kutokana na matukio ya kutisha
Baadhi ya waandishi wa habari wamelazimika kuhamisha maakazi yao hususani wale wanaoishi Darfur, kutokana na matukio ya mara kwa mara ya waandishi kutekwa na kuteswa na waasi.
Kwa mujibu wa Muungano wa Waandishi wa Habari wa Sudan, tangu kuanza kwa mapigano hayo, jumla ya waandishi wa habari 28 wameshauawa huku makumi ya wengine wakiwa kizuizini na kuteswa.
Soma pia: Mkuu wa haki wa UN ashtushwa na mauaji ya kiholela Sudan
"Nimepoteza mawasiliano yangu yote na wahariri na hata ofisi yangu walihamisha makaazi na kwenda Cairo. Nilishawahi kukamatwa na kuteswa sana hivyo nalazimika kufanya kazi kwa usiri mkubwa. " Anasema mwandishi wa habari wakati akihojiwa na shirika la habari la AFP.
Mbali na mateso wanayokutana nayo ya kuvamiwa, kutekwa na kuuawa, sasa mawasiliano ya simu na mitandao yamekatwa hali inayowalazimu waandishi wa habari kukimbilia kwemye milima mpakani mwa Chad na Sudan ili kupata mawasiliano.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Waandishi Wasio na Mipaka, jumla ya waandishi wa habaro 400 waliokwenda kuripoti mapigano hayo wamelazimika kuikimbia nchi hiyo.
Takwimu zinaonesha kuwa kwa mwaka jana, Sudan ilishika nafasi ya pili baada ya Gaza kwa matukio ya ukatili dhidi ya waandishi wa haabri.
Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, linasema makumi kwa maelfu ya raia wameuawa, zaidi ya milioni 12 wamegeuka wakimbizi, wakiwemo takribani milioni nne waliokimbilia nje ya nchi.