Vyombo vya habari Burundi vyakemea kuteswa kwa wanahabari
5 Mei 2025Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, wakurugenzi wa vyombo vinane vya habari vya kibinafsi nchini Burundi walitia saini taarifa ya pamoja wakielezea "wasiwasi wao mkubwa kuhusu vitendo vya vitisho wanavyofanyiwa waandishi wa habari".
Soma pia: Burundi yatoa orodha ya wahanga wa migogoro mbalimbali
Hii ni mara ya kwanza kwa waandishi wa habari mashuhuri kupaza sauti kwa pamoja nchini Burundi tangu mwaka 2015, wakati mzozo wa kisiasa ulisababisha vyombo kadhaa vya habari kufungwa huku karibu waandishi 150 wakilazimika kuikimbia nchi hiyo ndogo ya Afrika Mashariki. Katika taarifa yao ya Jumamosi, viongozi hao wa vyombo vya habari nchini Burundi wamesema hali inazidi kuwa mbaya kwa wanahabari hasa kabla ya uchaguzi wa bunge uliopangwa kufanyika Juni mwaka huu.
Burundi inashika nafasi ya 125 kati ya nchi 180 katika viwango vya uhuru wa vyombo vya habari vilivyotangazwa na Shirika la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka (RSF), ambalo limesema kuwa kumekuwa kukishuhudiwa mazingira "ya chuki kwa waandishi wa habari" nchini humo.