Vyanzo: Waasi wa M23 wameingia mji wa Bukavu
17 Februari 2025Hayo yameripotiwa na mashirika kadhaa ya habari yakimnukuu moja ya viongozi wa kundi hilo Corneille Nangaa huku wakaazi wa Bukavu wakisema wamewaona waasi hao kwenye mitaa ya wilaya ya kaskazini mwa mji huo.
Nangaa amesema wapiganaji wa M23 wameingia Bukavu ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini na hii leo wataanza "zoezi la kuusafisha mji huo."
Mapema hapo siku ya Ijumaa waasi hao waliukamata uwanja wa ndege muhimu wa Kavumu kaskazini mwa Bukavu. Jeshi la Kongo lilitangaza kukamatwa kwa uwanja huo wa ndege na kusema askari wake wamerudi nyuma wakiwa na vifaa vyao.
Vyanzo vimesema M23 wameingia mji wa Bukavu ulio na wakaazi wanaokaribia milioni 1 bila kukabiliana na upinzani wowote. Wakati waasi hao wanakaribia Bukavu, maduka na biashara zilifungwa na waakazi walianza kuukimbia mji huo.
Kukamatwa kwa mji huo ni mafanikio ya hivi karibuni kabisa ya M23 upande wa mashariki na ni pigo kwa utawala wa Rais Felix Tshisekedi, ambaye anakabiliwa na shinikizo la kufanya mazungumzo na kundi hilo. Kundi hilo tayari linaudhibiti mji mkubwa zaidi mashariki mwa Kongo wa Goma.
Mji wa Bukavu uliwahi kuangukia mikononi mwa wanajeshi walioliasi jeshi la Kongo mwaka 2004 na kukamatwa kwake hivi sasa kunalipa kundi la M23 udhibiti wa eneo kubwa la Ziwa Kivu, linalotandaa kwenye mpaka kati ya Kongo na Rwanda.
Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika lajadili mzozo wa Kongo bila Tshisekedi
Hayo yakijiri wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Afrika lilikutana kwa kikao maalumu mjini Addis Abbaba kuujadili mzozo wa Kongo.
Rais Tshisekedi hakuhudhuria kikao hicho na badala yake aliwakilisha na waziri mkuu.
Ofisi ya Tshisekedi imesema pia kiongozi huyo hatohudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afria unaoanza leo ili kushughulikia hali inayoshuhudiwa nchini mwake.
Mapema hapo jana ofisi hiyo ilitangaza Tshisekedi angekwenda Addis lakini mipango hiyo ilitolewa kabla ya taarifa za kuanguka kwa mji wa Bukavu.
Kabla ya kikao cha jana Ijumaa kuhusu Kongo mjini Addis, Mwenyekiti ayemaliza muda wake wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, aliliambia shirika la habari la AFP kwamba "usitishaji mapigano lazima uheshimiwe."
Alisema mapigano ya kijeshi yanayoendelea hayatotatua matatizo yanayoshuhudiwa na kwamba "huo ni mtazamo unaokubalika na wengi barani Afrika."
UNHCR yasema inatiwa wasiwasi na hali mbaya ya kiutu mashariki mwa Kongo
Katika hatua nyingine, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi UNHCR limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali inayozidi kuwa mbaya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, likisema, likisema vita katika eneo hilo limewaacha takriban watu 350,000 bila makazi.
Msemaji wa UNHCR Eujin Byun, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia ya video kwamba takriban wakimbizi 350,000 wa ndani hawana makazi kwasababu kambi zao za muda zimeharibiwa ama kuwepo kwa mabomu ambayo hayajaripuka kufanya kuwa hatari kwao kurudi nyumbani.
Kulingana na UNHCR, takriban asilimia 70 ya kambi katika eneo la Goma zimeharibiwa pamoja na nyingine huko Minova.
Byun ameongeza kuwa maelfu ya watu sasa wanaishi kwenye kambi za muda ikiwa ni pamoja na makanisa na hospitali.
Shirika hilo pia limeripoti kuongezeka kwa visa vya uhalifu na kusema hatari ya magonjwa inazidi kuongezeka huku likijitahidi pamoja na mashirika mengine kutoa msaada wakati mapigano yanaendelea.