Vyama vya ukombozi Afrika vyajadili kuikabili migogoro
28 Julai 2025Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania Mizengo Kayanza Peter Pinda aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa bara la Afrika kushikamana, akiongeza kuwa huu ni wakati wa kuhuisha maono ya waasisi kwa kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni baina ya mataifa ya Afrika.
Amesema "Lazima tuimarishe mshikamano ndani ya Afrika. Afrika iliyogawanyika ni Afrika dhaifu. Ikiwa vyama vyetu havitasimama pamoja, maslahi ya mataifa ya kigeni yataendelea kunufaika na migawanyiko yetu."
Naye Rais wa Namibia, Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, amesema ingawa Afrika imepata uhuru wa kisiasa, mateso ya watu wa Sahara Magharibi na Palestina yanaonesha kuwa mapambano ya ukombozi bado hayajakamilika. Amesema SWAPO kitaendelea kuunga mkono jitihada za mataifa hayo na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kukomesha dhuluma hizo.
"Ninarudia kusisitiza mshikamano thabiti wa Chama cha SWAPO na mapambano yao, na kutaka hatua ya haraka ya kimataifa ili kumaliza mateso na dhuluma wanazokumbana nazo watu wa Sahara Magharibi na Palestina," alisema Dkt. Nandi-Ndaitwah.
Rais wa Zimbabwe, Emerson Mnangagwa, amesisitiza kuwa historia ya ukombozi ni somo muhimu kwa Afrika. Amesema mamilioni ya watu wanaotegemea vyama vya ukombozi kwa matumaini ya maisha bora wanapaswa kuwa msukumo kwa viongozi na wananchi.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini yeye amebainisha kuwa harakati za ukombozi zilizaliwa katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi na ukoloni, na sasa zinapaswa kuibuka upya kwa lengo la kuleta umoja wa kikanda, ujumuishaji na uhuru wa mataifa katika mazingira magumu ya kisiasa na kiuchumi duniani.
Mbali na Tanzania na Angola ambazo marais wake wamewakilishwa, wakuu wa mataifa ya Msumbiji, Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia walihudhuria na wamesisitiza kuwa mshikamano wa vyama vya ukombozi bado ni muhimu sana katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kisiasa barani Afrika.