Ujerumani yapitisha mpango mpya wa matumizi ya fedha
15 Machi 2025Kansela mtarajiwa wa Ujerumani Friedrich Merz amesifu makubaliano yaliyoafikiwa na vyama vinavyowakilishwa katika bunge la Ujerumani Bundestag kupitisha mpango maalumu wa kihistoria wa fedha kwa ajili ya miundombinu na ulinzi wa thamani ya dola bilioni 500.
Akizungumza mjini Berlin, Merz alisema makubaliano hayo kati ya muungano wa vyama ndugu vya Christian Democratic Union, CDU na Christian Social Union, CSU, unaoongozwa na Merz, pamoja na chama cha Social Democtratic SPD na chama cha Kijani, unatuma ujumbe wa wazi kabisa kwa marafiki na maadui kote ulimwenguni kwamba katika siku za usoni hakutakuwa na uhaba wa raslimali za fedha kuulinda uhuru na amani.
Merz aliongeza kusema Ujerumani imerejea na kwamba ameridhishwa sana na matokeo hayo.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema hatua hiyo ni ishara kwa Ukraine, Ulaya na ulimwengu, akiongeza kwamba Ujerumani ilikuwa ikiwajibika huku kukiwa na changamoto za kimataifa.