Vyama vya Ujerumani vyafikiria kukopa zaidi
14 Februari 2025Ukosefu wa fedha tayari umesababisha changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kuvunjika kwa muungano wa serikali uliopita ulioundwa na Social Democrats (SPD), chama cha Kijani cha Ujerumani, na chama cha kiliberali FDP. Wakati bajeti ya mwaka 2025 ilipokuwa ikipangwa, kulikuwa na upungufu wa Euro 25 bilioni.
SPD na chama cha Kijani walitaka kufidia pengo hilo kwa kukopa, huku FDP ikikataa madeni mapya kabisa na kupendelea kupunguza matumizi ya kijamii. Muungano huo ulisambaratika Novemba 2024 baada ya vyama hivyo kushindwa kufikia makubaliano.
Hivyo basi, Ujerumani haina bajeti ya mwaka 2025. Kuipitisha itakuwa moja ya kazi za kwanza za serikali mpya. Hata hivyo, haitakuwa rahisi kwani vyama ambavyo, kulingana na kura za maoni, vina uwezekano wa kuunda muungano mpya havina mtazamo sawa kuhusu masuala ya fedha za umma.
Breki ya madeni ya Ujerumani ni nini?
Kifungu cha 115 cha Katiba ya Ujerumani kinaeleza kwamba "mapato na matumizi lazima yawe na uwiano bila kutegemea mikopo" - kwa maneno rahisi, serikali inaweza kutumia tu kiasi cha fedha inachokusanya. Breki ya madeni inaruhusu mikopo ya hadi asilimia 0.35 ya Pato la Taifa (GDP) pekee. Isipokuwa katika hali za dharura kama majanga ya asili au mgogoro mkubwa wa kiuchumi, sheria hii hairuhusu serikali kuchukua madeni makubwa.
Hata hivyo, mapato ya kodi hayatoshi tena kugharamia matumizi yanayokaribia. Serikali ya Ujerumani inakabiliwa na gharama kubwa, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa bajeti ya ulinzi, msaada kwa Ukraine, ukarabati wa miundombinu iliyoharibika, mabadiliko ya nishati kuelekea mfumo wa hali ya hewa usio na uchafuzi, na mchakato wa kidijitali ambao unakwenda taratibu.
CDU/CSU na FDP Zinataka Kudumisha Breki ya Madeni
Muungano wa vyama vya mrengo wa kulia vya CDU/CSU na chama cha FDP wanapinga kulegeza sheria hii ya ukomo wa deni. Mgombea wa Ukansela wa CDU/CSU, Friedrich Merz, alielezea wasiwasi wake katika mdahalo wa televisheni na Kansela Olaf Scholz mnamo Februari, akisema: "Tunataka kwenda umbali gani na deni letu? Ninaamini kuwa tuna jukumu kwa watoto wetu, ambao hatimaye watapaswa kulilipa."
Soma pia: Mazingira vs. uchumi: Je, Ujerumani inapaswa kuchagua?
Mnamo mwaka 2024, serikali ya Ujerumani ilikusanya takriban Euro 440 bilioni kutokana na kodi, huku jumla ya mapato ya serikali kuu, majimbo, na manispaa ikifikia Euro 960 bilioni. Merz alisisitiza kuwa: "Kimsingi, tunapaswa kufikia hatua ambapo tunaweza kuendesha serikali kwa kutumia mapato tunayokusanya kupitia kodi nchini Ujerumani."
Scholz ataka kuongeza deni
SPD na chama cha Kijani, ambavyo vinaweza kuunda muungano na CDU/CSU, vinapendekeza kurekebisha Kifungu cha 115 cha katiba ya Ujerumani. Olaf Scholz alisema katika kikao cha mwisho cha Bunge la Ujerumani (Bundestag) kabla ya uchaguzi wa Februari 23 kwamba: "Tunataka kuiboresha breki ya madeni kwa tahadhari."
Scholz amekuwa akisisitiza kwa miezi kadhaa kwamba Ujerumani inaweza kumudu deni kubwa zaidi. Alisema: "Marekani ina deni la kitaifa linalozidi asilimia 120 ya Pato la Taifa (GDP), wakati Ujerumani inakaribia asilimia 60."
Aliongeza kuwa mataifa mengine yenye uchumi imara kama Italia, Ufaransa, Uingereza, Canada, na Japani pia yana deni la kitaifa zaidi ya asilima 100 ya GDP.
Merz apinga hoja ya Scholz
Friedrich Merz, mgombea wa Ukansela wa CDU/CSU, hakubaliani na hoja hiyo. Alisema kuwa: "Itatulazimu kuweka vipaumbele vipya katika bajeti, ambayo inamaanisha hatuwezi kutarajia kila kitu."
Merz alipendekeza kupunguza ruzuku na ukubwa wa urasimu, na pia kupitia upya matumizi ya kijamii.
Alisema kwamba watu wengi zaidi wanapaswa kufanya kazi badala ya kutegemea misaada ya serikali: "Hizi ni akiba zinazowezekana ambazo tunahitaji kutumia."
CDU/CSU inatarajia kuwa mapato ya kodi yataongezeka kupitia ukuaji wa uchumi. Hata hivyo, Olaf Scholz anaita wazo hilo kuwa “la kipuuzi” kutokana na hali ya sasa ya uchumi.
Soma pia: Scholz na Merz wapambana kwa maneno bungeni
Katika ripoti yake ya kila mwaka kuhusu uchumi, serikali ya Ujerumani imetabiri kuwa uchumi utakua kwa asilimia 0.3 tu mwaka 2025 na asilimia 1.1 mwaka 2026.
Robert Habeck, Waziri wa Uchumi na mgombea wa Ukansela kwa tiketi ya chama cha Kijani, alisema katika Bundestag mwezi Januari kuwa hali hiyo haitabadilika hivi karibuni.
Chama cha Kijani kinatetea kuongeza deni
Chama cha Kijani (die Grüne) pia kinaamini kuwa hakuna njia nyingine ila kuongeza deni. Habeck alisisitiza: "Sisemi kuhusu kufuta breki ya madeni, wala sisemi kuhusu deni lisilo na kikomo," akiashiria kuwa hata wanauchumi wakuu, benki kuu ya Ujerumani (Bundesbank), na mashirika ya kimataifa kama OECD na IMF wanakubaliana kuwa uhuru zaidi wa kifedha unahitajika.
Habeck aliongeza: "Hatuwezi kuunda mustakabali kwa kutumia sheria kali ya breki ya madeni, iliyoanzishwa miaka ya 2000, wakati wa enzi tofauti, ambapo utandawazi ulikuwa unakua, hatukuwa na wasiwasi, na hapakuwa na vita barani Ulaya."
Ongezeko la matumizi ya kijeshi kwa Ujerumani na NATO
Matumizi ya kijeshi ni gharama inayoongezeka kila mara. Baada ya anguko la Ukuta wa Berlin na muungano wa Ujerumani, jeshi la Ujerumani (Bundeswehr) lilipunguzwa na ufadhili wake ukapungua polepole. Wakati wanachama wa NATO walikubaliana mwaka 2014 kutumia asilimia 2 ya Pato la Taifa (GDP) kwa ulinzi kila mwaka, Ujerumani ilikuwa mbali kufikia lengo hilo.
Baada ya uvamizi wa Urusi kwa Ukraine mnamo Februari 2022, Bundestag iliidhinisha mfuko maalum wa Euro 100 bilioni uliotokana na mkopo kwa ajili ya kuimarisha jeshi. Fedha hizo, zilizokusudiwa kusaidia bajeti ya kila mwaka ya ulinzi, zilipaswa kutumika kwa miaka kadhaa. Mnamo 2024, bajeti ya ulinzi ilikuwa Euro 52 bilioni, na ikaongezewa Euro 20 bilioni kutoka mfuko maalum.
Gharama za kijeshi zinazidi kuongezeka
Mfuko wa Euro 100 bilioni huenda ukawa umetumika ifikapo mwaka 2027, huku lengo la NATO la matumizi ya asilimia 2 ya GDP likitarajiwa kupanda. Kwa mujibu wa makadirio ya hivi karibuni, asilimia 3.6 ya GDP itahitajika kufanikisha malengo ya kijeshi ya muungano huo.
Soma pia: Uhakiki wa Ukweli: Je, madai ya Musk na Weidel yana ushahidi?
Kwa mujibu wa Ofisi ya Takwimu ya Shirikisho la Ujerumani, GDP ya Ujerumani mwaka jana ilikuwa Euro 4.3 trilioni. Ikiwa Ujerumani itatumia asilimia 2 ya GDP kwa ulinzi, itahitaji Euro 86 bilioni, na ikiwa asilimia 3.6 itahitajika, basi gharama itafikia Euro150 bilioni. Kwa kulinganisha, bajeti nzima ya shirikisho la Ujerumani kwa mwaka 2024 ilikuwa Euro 474 bilioni.
Scholz amesema kuwa ikiwa asilimia 2 ya GDP italazimika kutumiwa kwa ulinzi, basi Euro 30 bilioni zaidi zitahitajika kila mwaka kuanzia 2028. Aliongeza kuwa fedha hizo haziwezi kupatikana kirahisi tu "kwa pembeni."
Matumizi ya kijamii au uwekezaji?
Wakati wa kampeni za uchaguzi, Olaf Scholz ameonya dhidi ya kupunguza mafao ya uzeeni. Amesisitiza kuwa hataki usalama upambanishwe na mahitaji mengine, akisema: "Hatupaswi kupunguza huduma za kijamii, kupuuza reli, kutopanua barabara, au kuiacha miundombinu yetu iendelee kuoza."
Friedrich Merz alijibu kwa kusema: "Huu ni mtindo tunaojua kutoka kwa Social Democrats. Ikiwa hakuna pesa za kutosha, tunakopa zaidi, na ikiwa hatuwezi kustahimili deni kubwa zaidi, basi tunapandisha kodi."
Je, CDU/CSU wanataka kudumisha ukomo wa deni bila kujali gharama?
Wakati wa kampeni za uchaguzi, Friedrich Merz ameashiria kuwa anaweza kuwa na msimamo tofauti juu ya breki ya madeni. Katika mdahalo wa televisheni na Olaf Scholz, alisema: "Nimesema kwamba tunaweza kujadili kila kitu."
Hata hivyo, alisisitiza kuwa: "Kwanza kabisa, tunapaswa kutafuta maeneo ya kufanya akiba, kisha kukuza uchumi, na mwishowe kufanya marekebisho ya bajeti, ambayo yanahitajika kwa dharura."
CDU/CSU wameahidi kupunguza kodi kwa kiwango kikubwa katika ilani yake ya uchaguzi. Taasisi za utafiti wa uchumi zimekadiria kuwa mpango huu utazidisha nakisi ya bajeti kwa kati ya Euro 80 bilioni na Euro110 bilioni.
Kwa miaka mingi, mabadiliko katika breki ya madeni hayakuwa maarufu. Hata hivyo, kura za maoni zinaonyesha mtazamo wa Wajerumani umeanza kubadilika.
Utafiti wa Forsa, uliofanywa kwa agizo la Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Ujerumani (DGAP), umegundua kuwa asilimia 55 ya Wajerumani sasa wanaunga mkono marekebisho ya breki ya madeni au hata kuiondoa kabisa, huku asilimia 42 wakitaka iendelee bila kubadilishwa.