CDU/CSU na SPD vyatia saini makubaliano ya kuunda serikali
5 Mei 2025Wiki 10 baada ya uchaguzi wa mapema, viongozi wa vyama vya Christian Democratic (CDU), Christian Social Union (CSU), na Social Democratic (SPD) vya Ujerumani vimetia saini makubaliano yenye kurasa 144 yanayofungua njia kwa utawala mpya kuingia mamlakani. Baada ya makubaliano hayo yanayoainisha mpango wa namna ya kuongoza serikali, Friedrich Merz anatarajiwa kupigiwa kura na bunge Jumanne kuwa Kansela mpya.
Wakati wa hafla ya kusainiwa kwa makubaliano hayo Merz amesema, "Nchi hii inataka serikali inayofanya kazi kwa nguvu na kwa kufuata utaratibu tangu siku ya kwanza. Na hicho ndicho kitakachofanyika. Tuna mpango huo kwenye makubaliano ambayo tunayasaidi leo."
Vyama vitatu, vilivyoafikiana kushirikiana kuiongoza Ujerumani vya CDU, CSU na SPD vinadhibiti viti 328 katika bunge lenye viti 630. Merz, anayehitaji angalau viti 316 ana matumaini ya kutimiza kura zinazohitajika ili kuidhinishwa kuwa Kansela.
Merz amesema serikali inayoingia madarakani, imedhamiria kuipeleka mbele Ujerumani kwa kufanya mageuzi na uwekezaji. Ameahidi pia kuwa na serikali yenye sauti barani Ulaya na kote duniani.
Lars Klingbeil kushika nyadhifa za naibu wa Kansela na Waziri wa fedha
Katika serikali hiyo kiongozi mwenza wa chama SPD Lars Klingbeil anatazamiwa kuvaa kofia mbili, ya makamu wa Kansela na Waziri wa Fedha. Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius wa chama hicho cha Kansela anayemaliza muda wake Olaf Scholz ataendelea kushikilia wadhifa alionao katika serikali mpya. Waziri huyo ameshasema waziwazi kuwa Ujerumani inapaswa kujiandaa kwa vita kufikia mwaka 2029 kutokana na kitisho cha kiusalama kutoka Urusi.
Chama cha SPD kimempendekeza rais wa zamani wa bunge la Ujerumani Baerbel Bas, kuwa Waziri wa Kazi, Kamishna wa zamani wa Ujerumani Mashariki Carsten Schneider, kuiongoza wizara mpya ya mazingira na ulinzi wa tabianchi. Kimempendekeza pia Reem Alabali-Radovan, 35, kama Waziri wa Maendeleo.
Mara tu Merz atakapopitishwa kwa kura na bunge kuwa Kansela, na baraza lake la mawaziri litakapoapishwa, utawala mpya utaingia kazini ikiwa ni miezi sita baada ya serikali ya Kansela Scholz kuparaganyika.
Serikali mpya inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kusuasua kwa uchumi, kuzorota kwa miundombinu na kitisho cha usalama cha Urusi kwa Umoja wa laya.