CDU/CSU, SPD waanza mazungumzo ya awali ya kuunda serikali
28 Februari 2025Wawakilishi wakuu wa vyama hivyo wamekutana siku ya Ijumaa katika jengo la Bunge mjini Berlin. Mazungumzo ya leo Ijumaa ni ya kujadili kwanza ajenda kuu zitakazojadiliwa na kupanga ratiba ya mazungumzo ya kina ambayo hadi sasa haijafahamika yataanza lini.
Merz anadhamiria kuunda serikali kabla ya Jumapili ya Pasaka mnamo Aprili 20, ili kushughulikia changamoto lukuki zinazoikabili Ujerumani. Hata hivyo kiongozi wa SPD Lars Klingbeil amesisitiza kuwa masharti yote yanapaswa kuzingatiwa ili waweze kukubali kuunda serikali ya muungano.
Katika mazungumzo hayo ya awali, kila upande umetuma wapatanishi tisa watakaojadiliana kufuatia mkutano wa Jumanne wiki hii kati ya Merz na Scholz.
Soma pia: SPD tayari kwa mazungumzo ya 'dhati' na CDU
Kulingana na shirika la habari la Ujerumani DPA, ujumbe wa wahafidhina unamjumuisha Merz, anayeongoza CDU na Markus Söder mwenyekiti wa chama ndugu cha CSU. Timu ya SPD inajumuisha viongozi wenza wa chama hicho Klingbeil na Saskia Esken, Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius na Waziri wa ajira Hubertus Heil.
Mazungumzo ya muungano kati ya CDU/CSU na SPD yanatarajiwa kuwa magumu, kutokana na tofauti zao zilizo dhahiri kuhusu masuala kama vile uhamiaji, namna ya kufadhili bajeti na mzozo wa Ukraine. Mwanachama wa SPD na mkuu wa jimbo la Mecklenburg-Vorpommern, Manuela Schwesig amesema vyama vinavyoshiriki mazungumzo hayo vinapaswa kuelewana ili kufikia lengo la kuunda serikali:
"Pande zote mbili lazima ziafikiane. Tunapaswa sote kujumuika pamoja na kusonga mbele. Uaminifu unapaswa kupewa kipaumbele. Lazima tujifunze kwa yale yaliyotokea katika serikali iliyovunjika. Migogoro ya mara kwa mara haithiri tu wale wanaohusika, bali pia inaathiri demokrasia. Kinachohitajika ni msingi thabiti wa uaminifu na nia ya kutaka kufanya kazi pamoja. Msisitizo haupaswi kuwekwa katika faida za vyama, lakini katika kutatua matatizo makubwa, ambayo ni kuendeleza nchi kiuchumi, kuwahakikishia watu ustawi wa jamii na usalama wa kiuchumi."
Serikali ijayo itakabiliwa na changamoto lukuki
Kambi hiyo ya kihafidhina ya CDU-CSU inayoongozwa na anayetarajiwa kuwa Kansela ajaye wa Ujerumani Friedrich Merz , ilishinda uchaguzi kwa kujipatia asilimia 28.5 ya kura, huku chama cha SPD cha Kansela wa sasa Olaf Scholz kikiporomoka hadi asilimia 16.4 na kujikuta nafasi ya tatu nyuma ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Mbadala kwa Ujerumani (AfD), ambacho hakijaalikwa kushiriki mazungumzo hayo ya awali ya kuunda serikali.
Serikali ijayo ya Ujerumani itakabiliwa hata hivyo na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mdororo wa kiuchumi huku ripoti iliyotolewa hivi karibuni ikieleza kuwa idadi ya watu wasio na ajira imeongezeka nchini humo na kufikia jumla ya watu milioni 2.86.
Viongozi wajao wa taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya watakuwa pia na kibarua cha kushiriki kikamilifu kwenye michakato ya kushughulikia mizozo kama ile ya Ukraine na Mashariki ya Kati.
(Vyanzo: DPA, AP)