Vyama ndugu vya CDU/CSU na SPD kufikia makubaliano
10 Machi 2025Wajumbe wa Christian Democratic Union, CDU na Christian Social Union, CSU na wale wa SPD walipiga hatua wiki hii.
Katika mazungumzo ya awali, walikubaliana kuondoa vikwazo vya deni kwa matumizi ya ulinzi, ili kuliimarisha jeshi la Ujerumani Bundeswehr, na kurekebisha miundombinu inayosuasua.
Mazungumzo yanaendelea haraka. Vyama hivyo vimekuwa katika serikali pamoja hapo kabla, hasa hivi karibuni chini ya Kansela Angela Merkel hadi mwaka 2021. Kwa hivyo kuna mambo mengi wanayokubaliana, lakini pia kuna tofauti kubwa.
Vyama vya CDU/CSU na SPD vinakubaliana kuhusu uhitaji wa dharura wa kuwekeza na kuliimarisha jeshi la Ujerumani katika wakati ambapo Marekani inaonekana kuitupa mkono Ulaya. CDU/CSU inafikiria kurejesha tena huduma ya kujiunga na jeshi kwa lazima, ambayo ilisitishwa mwaka 2011.
Soma pia:Uchaguzi wa Bunge la Shirikisho: Matokeo yanamaanisha nini kwa uchumi?
Hata hivyo, SPD inaona kuwa uandikishaji wa watu wengi kama jambo lisilowezekana kudhibitiwa na wanashinikiza muundo wa kujiunga na jeshi uwe wa hiari.
Vyama vyote vya CDU/CSU na SPD vinakubaliana kwamba Ujerumani ina jukumu la kuendelea kuiunga mkono Ukraine.
Kiongozi wa CDU na kansela ajaye Friedrich Merz, mara kwa mara amezungumzia kuunga mkono kupelekwa kwa makombora yaliyotengenezwa Ujerumani chapa Taurus nchini Ukraine, jambo ambalo Kansela Olaf Scholz alikataa kulifanya, akidai kuwa makombora hayo ya masafa marefu yanaweza kuiingiza Ujerumani katika vita.
Uhusiano wa Ujerumani na Ulaya ni muhimu katika majadiliano
Vyama vyote vya CDU/CSU na SPD vimeshangazwa na jinsi Rais wa Marekani Donald Trump anavyoiangalia Ukraine, hatua yake ya kuitilia shaka Jumuiya ya Kujihami ya NATO, na nia yake ya kuzitoza ushuru bidhaa zinazoingia kutoka Ulaya.
Hata hivyo, Merz ameacha mlango wazi kwa utawala wa Trump, kuliko kiongozi wa SPD Lars Klingbeil. Merz bado anajaribu kuifanya Marekani ijihusishe na Ulaya na ana matumaini ya kufanikiwa kwa kuheshimu makubaliano ya usalama na Ukraine.
Uhamiaji ni moja ya masuala muhimu ya kuzingatia, CDU/CSU wanataka kuwepo sera Kali zaidi za uhamiaji ili kuzuia kile kinachoitwa wahamiaji wasio na vibali maalum.
Hii ni pamoja na kuwarejesha makwao wakimbizi katika mipaka ya Ujerumani bila kuzingatia kigezo maalum, wakiwemo wanaotafuta hifadhi.
SPD inaamini kuwa hilo haliendani na katiba ya Ujerumani wala sheria za Umoja wa Ulaya. Akizungumza na kituo cha televisheni cha ARD wiki hii, Klingbeil aliweka wazi kwamba chama chake cha SPD kitajadiliana kwa undani kuhusu suala hilo.
Soma pia:Ujerumani kuelekeza mabilioni ya yuro katika jeshi
Matumizi ya ustawi wa jamii yameongezeka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, hasa kutokana na kuingia kwa maelfu ya watu kutoka Ukraine. SPD inataka kuendelezwa kwa posho ya kujikimu ya kawaida kwa watu wasio na ajira.
CDU/CSU na Merz wanataka kuona mageuzi ya kimsingi ya ustawi wa jamii. Anapendekezan wale wanaokataa kufanya kazi wapunguziwe posho yao.
Kwa ujumla katika uchumi na kodi, SPD inaamini katika mpango wa serikali, ruzuku na uwekezajiili kuuchohea uchumi. Hata hivyo, CDU/CSU inakusudia kuzingatia zaidi kuhimiza uwekezaji binafsi kwa kupunguza kodi. Wanataka kupunguza ushuru wa kampuni kwa hatua hadi kiwango cha juu cha asilimia 25.
SPD kwa upande mwingine inataka kupunguza ushuru wa mapato kwa wastani wa asilimia 95 ya walipa kodi, huku watu wenye kipato cha juu wakilipa zaidi.
CDU/CSU haitaki kuachana na lengo la kupunguza hadi kiwango sifuri matumizi ya gesi inayochafua mazingira ifikapo mwaka 2045, lakini imeapa kuweka kipaumbele katika kuongeza ushindani kwenye sekta ya nishati Ujerumani.
CDU/CSU inataka hasa kusaidia sekta ya magari inayokabiliwa na matatizo ya kifedha na kuondoa marufuku ijayo ya Umoja wa Ulaya magari yanayotumia nishati ya mafuta. Muungano huo wa kihafidhina pia unafikiria kurejea kwenye nishati ya nyuklia.