Vurugu zauwa watu wawili baada ya ushindi wa PSG
1 Juni 2025Watu wawili wamepoteza maisha na mamia wamekamatwa usiku wa kuamkia leo Jumapili huko Ufaransa wakati wa shangwe za ushindi wa klabu ya Paris Saint-Germain wa finali za Champions League.
Wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa imesema watu 491 walikamatwa mjini Paris kufuatia vurugu zilizoibuka kati ya kundi kubwa la mashabiki waliokusanyika na maafisa wa usalama.
Kitovu cha hekaheka kubwa ya shangwe kilikuwa Paris ambako magari yalipiga honi,kelele,huku mashabiki wakiimba katika mitaa ya mji huo mkuu wa Ufaransa kufuatia ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Intermilan katika fainali iliyochezwa mjini Munich Ujerumani.
Soma pia: Fainali ya Champions League ni PSG vs Inter MilanMtu mmoja aliuwawa kwa kugongwa na gari kusini mwa Paris huku kijana wa miaka 17 naye akipoteza uhai kwa kuchomwa kisu katika mkusanyiko wa kusherekea ushindi huo wa PSG katika mji wa Dax Kusini Magharibi mwa Ufaransa.
Kufikia leo Jumapili imeelezwa kwamba jumla ya watu 559 wamekamatwa .
Polisi mjini Paris imesema vurugu kubwa zilizuka karibu na barabara ya Champs-Elysee na kwenye maeneo ya uwanja wa michezo wa PSG wa Parc des Princes ambako mashabiki 48,000 walikuwa wamefurika kuutazama mchuano huo kupitia televisheni kubwa, ulioishia kwa ushindi wa PSG.
Sherehe za gwaride kuikaribisha PSG
PSG inatarajiwa leo Jumapili kuandaa sherehe kubwa ya gwaride la ushindi kwenye eneo la Champs -Elysee ambapo maelfu ya mashabiki wake wanatarajiwa kukusanyika kujionea na kuwashuhudia mashujaa wao wa soka.Soma pia: Arsenal yapania kuipiku PSG nusu fainali ya ligi ya mabingwa
Ofisa ya raism Emmanuel Macron imesema kiongozi huyo atawakaribisha washindi hao kuwapongeza leo Jumapili. Jumla ya watu milioni 11.5 waliufuatilia mchuano huo kote nchini Ufaransa kupitia televisheni.