Vita vya Sudan miaka miwili baadae, hali bado ni mbaya
15 Aprili 2025Maafisa wa ngazi za juu, wanadiplomasia na viongozi wanakutana leo mjini London kujadiliana namna ya kuisadia Sudan kufikia amani baada ya kushuhudia vita kwa miaka miwili, vita vinavyohusisha jeshi la serikali na wanamgambo wa kundi la RSF.Ingawa kwenye mkutano huo wa London pande hizo zilizoko vitani hazikushirikishwa.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kabla ya mkutano huo, jana Jumatatu alizungumzia wasiwasi alionao kuhusu silaha zinazoendelea kuingia nchini Sudan pamoja na wapiganaji ,hali ambayo inaonesha uhalisia wa vita hivyo vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomaliza miaka miwili.
Guterres, bila ya kutaja nchi yoyote kwenye tamko lake hapo jana alisema lakini kwamba wale wenye ushawishi mkubwa kwenye vita vya Sudan wanapaswa kutumia ushawishi huo kuimarisha maisha ya raia wa taifa hilo na sio kuliongeza makali janga hili. Tayari maelfu ya watu wamekwishauwawa na mamilioni kuachwa bila makaazi na kutumbukia pia kwenye baa la njaa.
Na mashirika mbali mbali ya kibinadamu yamezungumzia kuhusu hali ilivyo Sudan. Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Fillipo Grandi ametahadharisha akisema, kuwapuuza wakimbizi waliokimbia vita vya Sudan kutasababisha athari kubwa.Soma Pia: Baada ya miaka miwili ya vita, Sudan bado haina dalili ya kufikia amani
Mamadou Duain Balde, ambaye ni mkurugenzi wa UNHCR kanda ya Afrika Mashariki, pembe ya Afrika na eneo la maziwa makuu amezungumzia kuhusu hali ilivyo kwa sasa katika maeneo hayo.
''Nchi kadhaa zimekuwa zikiwapokea wakimbizi. Nchi za Kikanda,Mataifa jirani hayakufunga mipaka yao. Yamekuwa yakiwapokea wakimbizi. Jamii ambazo hata hazina kikubwa cha kutoa, zimewagawia kidogo walicho nacho. Na huo ndio moyo wa kweli wa mshikamano. Na hiyo ndiyo hali tunayoiona inaendelea katika kanda hii''
Vita vya Sudan vilivyopewa jina ''Vita vilivyosahaulika'' kati ya jeshi la serikali na wanamgambo wa kundi la RSF ni vita vya kuwania madaraka baina ya majenerali wawili, AbdelFattah Al Burhan na Hamdani Dagalo.Soma pia: Sudan yageuka uwanja wa mapigano kwa wapiganaji wa kigeni
Phillipo Grandi mkuu wa UNCHR amesema miaka miwili ya vita imetengeneza kile ambacho hivi sasa ulimwengu unakishuhudia,ambacho ni mgogoro mkubwa wa kibinadamu na wakimbizi na kuongezeka kwa hatua za kupunguzwa kwa msaada wa kimataifa.
Mkutano wa London kwa hivyo unawashirikisha pia maafisa wa mashirika ya msaada,na wanadiplomasia kutoka mataifa mbali mbali ya ulimwengu. Mkutano huo wa siku moja, hii leo Jumanne umeandaliwa na Uingereza,Ufaransa,Ujerumani na Umoja wa Ulaya pamoja na Umoja wa Afrika,lengo lake kubwa ni kujaribu kupata ufumbuzi wa kuondowa kile ambacho Umoja wa Mataifa umekiita, "mgogoro wa kutisha wa Kibinadamu duniani."