Vita kati ya Ukraine na Urusi bado kizungumkuti
2 Februari 2025Jeshi la anga la Ukraine limesema leo Jumapili kwamba mifumo yake ya ulinzi wa anga imezidungua droni 40 kati ya 55 zilizorushwa na Urusi usiku wa kuamkia leo katika mwendelezo wa mashambulizi baina ya nchi hizo mbili.Taarifa hiyo ya kijeshi imeongeza kwamba droni 13 zilipotea na hazikuweza kuyafikia maeneo yaliyolengwa.
Mamlaka nchini Ukraine zimesema mashambulizi mengine ya Urusi yaliyofanyika hapo jana yaliwaua watu 11 na kujeruhi wengine 16 na kufanya uharibifu wa majengo ya makaazi ya watu katika mji wa Poltava.
Soma zaidi.
Katika mtandao wa kijamii wa X, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameishutumu Urusi kwa kufanya mashambulizi hayo katika makaazi ya watu na kutoa wito kwamba lazima Urusi ilazimishwe kusitisha mashambulizi ya aina hiyo.
Mzozo baina ya nchi hizo mbili una karibu miaka mitatu sasa na bado unaendelea kuchukua mkondo mpya kila siku kwa mashambulizi mapya ya droni na makombora kutoka kwa pande zote mbili.