Viongozi wenyeji wahusishwe katika utawala wa maji
24 Agosti 2006Wachunguzi wa taasisi ya amani ya mjini Bonn wameshtushwa na majibu walioyapata kuhusu ripoti yake mpya. Serikali nyingi za nchi za Kiafrika zilipeleka ombi la kupata nakali nyingi za ripoti inayohusu njia za kuzuia mizozo ya maji katika maeneo ya mpakani. Barani Afrika mito mingi inatumika na nchi kadhaa kama vile mto wa Nile. Pia, maeneo makubwa ya Afrika yanakabiliwa na ukosefu wa maji.
Sababu kuu ya tatizo la maji barani Afrika lakini si ukosefu hawa wa maji, bali utawala na siasa mbaya, anasema Volker Böge, mtungaji wa ripoti mpya iliyochapishwa karibuni. Lakini hata iwapo serikali inashindwa kuweka utawala bora wa maji, haina maana kwamba utawala wa maji haupo kabisa. Yaani badala ya idara za kiserikali, vijiji vyenyewe vinasimamia matumizi ya maji.
Volker Böge anaeleza: “Nchini Tanzania na kwenye nchi nyingine kuna mifano mingi ya serikali zilizoanzisha vikundi rasmi vya watumizi wa maji, lakini wakaazi tayari walikuwa na utaratibu wao wa kugawa maji. Halafu tena utaratibu wa kiserikali unaleta kazi nyingi za kujaza mafomu na mambo kama hayo.”
Ikiwa ni serikali au mashirika ya kimataifa ambayo yanajihusisha zaidi na kuweka utawala bora wa maji katika nchi zinazoendelea, wote wanasahau kwamba viongozi wa mashinani wana jukumu pia katika suala hilo: “Familia na ukoo una umuhimu katika maeneo ya mashambani barani Afrika, kwa hivyo viongozi wa kienyeji, ikiwa ni chifu wa kijiji au waganga, wana usemi katika masuala ya utawala wa maji. Lakini hawazingatiwi katika katiba au sheria zinazohusu maji ya nchi hizo.”
Hususan katika maeneo ya mipaka, mchunguzi huyu anataka jamii ya wenyeji na utaratibu wao wa kugawa maji upewe uzito. Kwani katika mwahala mwingi, watu wa kabila moja wanaishi kwenye pande zote za mto ambao ni mpaka. Licha ya kuwa raia wa nchi mbili wanaafikiana juu ya matumizi ya maji ya mto huo.
Bw. Böge alitoa mfano wa kabila la Wahimba wanaoisha mpakani mwa Namibia na Angola na ambao wanakubaliana juu ya matumizi ya mto wa Kunene ambao unawagawa – bila ya kujali mpaka rasmi. Volker Böge anasema: “Ingawa maafikiano haya hayazishughulishi serikali za nchi hizi mbili, juu ya hivyo ni kama siasa ya kimataifa ya utawala wa maji. Lakini kwenye mikutano ya kimataifa mifano hiyo haizungumziwi.”
Kwa sababu hiyo, Bw. Böge amefunga safari hadi Stockholm kuiwasilisha ripoti yake mbele ya wataalum wa mambo ya maji, ili mifano hiyo inaweza kuwa masomo mazuri kwa maeneo mengine duniani.