Ukraine yaadhimisha miaka mitatu ya uvamizi wa Urusi
24 Februari 2025Rais Volodymyr Zelensky hii leo ametoa wito wa kupatikana kwa amani ya kudumu na endelevu nchini Ukraine mwaka huu, katika maoni yake ya kuadhimisha miaka mitatu ya uvamizi wa Urusi.
Amesema mwaka huu unapaswa kuwa mwanzo wa amani ya kweli na ya kudumu na kuongeza kuwa Rais Vladimir Putin wa Urusi hataweza kufanya hivyo, akisisitiza amani inaweza kupatikana kwa hekima na mshikamano.
Viongozi kadhaa wa Ulayana Canada wako nchini Ukraine kwa ajili ya maadhimisho hayo na kuonyesha mshikamano na taifa hilo, ikiwa ni pamoja na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau.
Viongozi wengine wanaotarajiwa kwenda Ukraine ni Rais wa Baraza la Ulaya Antonio Costa na mawaziri wakuu wa mataifa ya magharibi mwa Ulaya pamoja na Uhispania, ambao watajadiliana na Rais Zelenskyy kuhusu mabadiliko ya sera ya Rais Donald Trump kuelekea vita hivyo.