Viongozi walaani shambulizi la Israel kwenye hospitali Gaza
26 Agosti 2025Maafisa wa afya wa Gaza wamesema shambulizi hilo kwenye hospitali ya Nasser huko Khan Younis liliwauwa watu 20 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 80.
Ni miongoni mwa mashambulizi mabaya zaidi ya Israel ambayo yamezikumba hospitali na waandishi wa habari katika vita vilivyodumu kwa miezi 22.
Shambulio hilo lilijiri wakati Israel ikipanga kupanua mashambulizi yake kwenye maeneo yenye wakazi wengi, ikiapa kuwaangamiza Hamas baada ya shambulio lake la Oktoba 7, 2023.
Miongoni mwa waliouawa ni waandishi Habari watano, akiwemo Mariam Dagga, mpiga picha wa shirika la Habari la AP, mwenye umri wa miaka 33. Shirika la Habari la Reuters lilisema mmoja wa maripota wake aliuawa katika shambulizi la mwanzo wakati akipiga picha za moja kwa moja za televisheni kwenye ghorofa ya juu ya hospitali ya Nasser huko Khan Younis.
Waandishi wengine, akiwemo Dagga, na wafanyakazi wa uokozi walikuwa wamevalia vizibao vya chungwa vya huduma za dharura wakati walipolipuliwa katika shambulizi la pili walipokuwa wakipanda ngazi za jengo hilo kwenda kwenye eneo la mkasa.
Israel yasema inachunguza
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameliita shambulizi hilo kuwa la "bahati mbaya” na kusema jeshi linalichunguza. Alisema Israel inajutia tukio hilo na kwamba inathamini kazi ya waandishi, wahudumu wa afya na raia wote.
Brig. Jen. Effie Defrin, msemaji wa jeshi la Israel, amesema jeshi huwa haliwalengi raia na kwamba limeanzisha uchunguzi wa ndani kuhusu mashambulizi hayo. Aliwahutumu Hamas kwa kujificha miongoni mwa raia lakini hakusema kama Israel iliamini wanamgambo wowote walikuwepo wakati wa mashambulizi kwenye hospitali hiyo.
"Mkuu wa Majeshi ameagiza uchunguzi ufanywe mara moja ili kuelewa mazingira ya kile kilichotokea na jinsi kilivyotokea. Kuripoti kutokea eneo la vita kuna hatari kubwa, hasa katika vita na kundi la kigaidi kama vile Hamas, ambalo linajificha nyuma ya raia. Kama kawaida, tutawasilisha matokeo ya uchunguzi wetu kwa uwazi iwezekanavyo." Alisema Defrin.
Israel imewauwa waandishi 189 wa Kipalestina wakati wa kampeni yake Gaza, wakiwemo baadhi waliolengwa moja kwa moja na wengine waliouawa miongoni mwa mashambulizi ya jumla kwa mujibu wa Kamati ya Kuwalinda Waandishi – CPJ. Umoja wa Mataifa unasema Zaidi ya wahudumu wa afya 1, 500 wameuawa mpaka sasa.
Jumuiya ya Kimataifa yalaani shambulizi
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Uingereza, Ufaransa na madola mengine wamelaani shambulizi hilo. Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric anasema "Katibu Mkuu anasistiza kuwa raia, wakiwemo wahudumu wa afya na waandishi habari, lazima waheshimiwe na kulingwa wakati wote. Ametoa wito wa uchunguzi wa haraka, na usioegemea upande wowote kuhusu mauaji hayo."
Rais wa Marekani Donald Trump alisema anadhani mgogoro wa Gaza huenda ukahitimishwa katika wiki chache zijazo, bila kufafanua. Haikuwa wazi kama alimaanisha operesheni inayoanza ya Israel au kuhusu mazungumzo ya muda mrefu ya kusitisha mapigano.
Ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema waandishi na hospitali hazifai kulengwa. Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya Wapalestina UNRWA, Philippe Lazzarini, alielezea shambulizi hilo kuwa la "kunyamazisha sauti za mwisho zilizosalia ambazo zinaripoti kuhusu watoto wanaokufa kimyakimya huku kukiwa na baa la njaa.”
Nchini Qatar, ambayo imekuwa ikijaribu kusimamia mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza, wizara ya mambo ya nje ililaani shambulizi hilo ikisema ni "tukio jipya katika mfululizo wa matukio yanayoendelea ya uhalifu wa kutisha" wa Israel.
Shirika la hisani la Madaktari wasio na mipaka – MSF limesema "limevunjwa moyo” na kifo cha mpiga picha wa kujitegemea Mariam Abu Dagga ambaye wakati mmoja aliwahi kulifanyia kazi.
AP, AFP, Reuters