Viongozi wa ulimwengu wampongeza Papa Leo XIV
9 Mei 2025Prevost amelichagua jina la Papa Leo XIV. Anakuwa papa wa kwanza katika historia kutokea Marekani. Baada ya kuchaguliwa, alijitokeza hadharani kwa mara ya kwanza kwenye roshani ya Kanisa la Mtakatifu Petero mwendo wa saa moja na dakika 13 jioni saa za Rome. Alishangiliwa kwa vifijo na zaidi ya watu 100,000 waliokuwa wakisubiri kwa hamu.
Alihutubia katika Kitaliano. "Ndugu wapendwa, hizi ni salamu yangu ya kwanza a Kristo Aliyefufuka, Mchungaji Mwema, aliyetoa maisha yake kwa ajili ya kondoo wa Mungu. Nami pia ningependa salamu hii ya amani iingie mioyoni mwenu na izifikie familia zenu, watu wote, popote walipo, mataifa yote, dunia nzima. Amani iwe nanyi."
Papa Leo XIV awali alihudumu katika makao makuu ya Kanisa mjini Vatican, akiiongoza wizara inayosimamia maaskofu kote ulimwenguni. Mapema katika taaluma yake, alihudumu kama mmishonari na askofu nchini Peru.
Papa Leo, anayezungumza Kiitaliano na Kihispania, pia aliuhutubia umati uliokuwa kwenye viwanja vya kanisa hilo akitumia Kihispania katika maneno yake ya kwanza akiwa kiongozi wa Wakatoliki bilioni 1.4 ulimwenguni. "Nanyi pia, mtusaidie kisha msaidiane miongoni mwenu , kujenga madaraja kwa njia ya mazungumzo, kwa kushirikiana, kutuunganisha sisi sote kuwa watu wamoja, daima kwa amani."
Leo XIV anakuwa papa wa 267 katika historia ya miaka 2,000 ya Kanisa Katoliki.
Salamu za pongezi zatolewa
Viongozi wa ulimwengu wametuma salamu za kumpongeza papa kwa kuchaguliwa kwake. Miongoni mwa waliokuwa wa kwanza kumpongeza papa mpya ni Rais wa Marekani Donald Trump aliyesema ni heshima kwa taifa la Marekani kumpata Papa wa kwanza Mmarekani.
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, ambaye ni Mkatoliki alisema watu nchini Ujerumani wanautizama uongozi mpya wa papa kwa imani na matarajio chanya. Wengine waliompongeza ni Waziri Mkuu wa Italia Georgia Meloni, Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen marais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Vladmir Putin wa Urusi.