Viongozi wa Ulaya wakutana Brussels
26 Juni 2025Mkutano huu unafanyika siku moja baada ya mkutano wa kilele wa NATO huko The Hague, ambapo nchi wanachama ziliahidi kuongeza matumizi ya ulinzi hadi asilimia 5 ya pato ghafi la taifa.
Katika muktadha wa vita vya Ukraine, viongozi hao wanajadili duru ya 18 ya vikwazo dhidi ya Urusi na mustakabali wa kikomo cha bei ya mafuta ya Urusi — hatua ambazo baadhi ya nchi, kama Hungary na Slovakia, zimekuwa zikizipinga kwa hofu ya athari za kiuchumi. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky anatarajiwa kujiunga na kikao hicho kwa njia ya video, ikiwa ni siku moja baada ya kukutana ana kwa ana na Rais Donald Trump nchini Uholanzi.
Orban aendelea kupinga msaada zaidi kwa Ukraine
Waziri Mkuu wa Hungary, Viktor Orbán, ameendelea kupinga msaada zaidi kwa Ukraine na juhudi zake za kujiunga na Umoja wa Ulaya, akidai hatua hiyo itachochea vita barani Ulaya. Kwa upande wake, Rais Gitanas Nauseda wa Lithuania amesisitiza kuwa Ukraine imetimiza vigezo vyote vya mageuzi, na anasikitishwa na kucheleweshwa kwa mchakato huo.
Katika mjadala kuhusu hatma ya biashara kati ya EU na Marekani, Waziri Mkuu wa Ireland Micheal Martin amesisitiza umuhimu wa kufikia makubaliano ya kibiashara kabla ya mwisho wa muda uliowekwa na Rais Donald Trump. Amesema hatua hiyo ni muhimu kwa utulivu wa kiuchumi barani Ulaya na kwa maslahi ya wafanyakazi na wawekezaji.
"Kila mtu ndani ya Umoja wa Ulaya analenga kufikia makubaliano ya mazungumzo na Marekani kabla ya Julai 9, jambo ambalo ni muhimu sana kwa masoko, wawekezaji, wafanyakazi na sekta ya viwanda. Tunapaswa kufanya kila juhudi kupata suluhu inayokubalika. Si suluhisho bora, lakini hatutaki ushuru wa forodha – ingawa tunalazimika kukabiliana na hali ilivyo mbele yetu.”
Mzozo wa Gaza watupiwa jicho
Mkutano huo pia unajadili mzozo wa Mashariki ya Kati, ambapo Rais wa Baraza la Ulaya António Costa ametoa wito wa kujizuia, kuheshimu sheria za kimataifa na kuhimiza suluhu ya kidiplomasia. Waziri Mkuu wa Luxembourg Luc Frieden, naye, amesema hali ya kibinadamu Gaza ni ya kusikitisha na haki za Wapalestina haziwezi tena kufumbiwa macho.
Hata hivyo, suala la Gaza limewagawanya viongozi wa EU. Baadhi wanapendekeza msimamo mkali dhidi ya Israel, huku baadhi wakitaka tahadhari zaidi katika kulinda ushirikiano wa kidiplomasia. Mgawanyiko huu unaendelea kuzua maswali kuhusu uwezo wa EU kuwa na msimamo wa pamoja.
Masuala ya mazingira pia yako mezani, huku viongozi wakijadili lengo lililocheleweshwa la kupunguza utoaji hewa chafu kufikia mwaka 2040. Tofauti kuhusu muda na kiwango cha kupunguza uzalishaji wa kaboni zinaendelea kugawanya mataifa wanachama.
Pamoja na changamoto hizi, mkutano wa Brussels umeweka wazi haja ya maamuzi ya haraka na mshikamano wa kisera — hasa wakati ambapo nafasi ya Umoja wa Ulaya katika jukwaa la kimataifa inapimwa dhidi ya ushawishi wa Marekani, mvutano wa kiuchumi, na migogoro ya kijeshi inayotikisa dunia.