Viongozi wa Ulaya wakutana London kuujadili mzozo wa Ukraine
12 Mei 2025Mawaziri wa Mambo ya Nje wanaokutana London leo hii ni kutoka nchi sita za Ulaya zilizopo kwenye muungano unaojulikana Weimar+ unaozijumuisha Uingereza, Ufaransa, Italia, Ujerumani, Uhispania na Poland. Viongozi hao walipokelewa na mwenyeji wao wa Uingereza David Lammy aliyemtaka rais wa Urusi Vladimir Putin kuliwekea umuhimu suala la kushiriki katika mazungumzo ya amani na kumpongeza rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwa utayari wake.
Zelensky alisema yuko tayari kukutana ana kwa ana na Putin nchini Uturuki siku ya Alhamisi baada ya Kremlin kutoa pendekezo hilo la pande hizo kufanya mazungumzo mjini Istanbul. Kremlin lakini haikupendekeza mkutano wa ngazi ya juu kati ya Rais Putin na Zelenskyy. Hata hivo Lammy amesema Ulaya imejiandaa iwapo Putin hatoonyesha nia ya dhati ya kushiriki mchakato huo wa amani.
Alipowasili mjini London kushiriki mkutano huo, Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas ameelezea kwa uchache yale yatakayojadiliwa:
"Leo tutajadili mada muhimu sana, ikiwa ni pamoja na uhusiano baina ya Umoja wa Ulaya na Uingereza, na bila shaka kile kinachoendelea nchini Ukraine na namna tunavyoweza kufikia mpango wa usitishaji mapigano na mwishowe kupatikane amani. Ili kuanzisha mazungumzo yoyote ya amani, ni lazima kuwepo na usitishaji vita."
Ufaransa na Ujerumani zatishia kuzidisha vikwazo kwa Urusi ikiwa itakaidi miito ya amani
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ni lazima nchi za Ulaya zizidishe vikwazo dhidi ya Urusi ikiwa haitaki amani. Mawaziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Noel Barrot na yule wa Ujerumani Johann Wadephul wamefikiana huko London kuzidisha shinikizo kwa Urusi ikiwa itaendelea kukaidi miito ya usitishwaji mapigano.
Msemaji wa Kremlin Dmitry Peskov amesema leo bila kutoa maelezo zaidi kwamba rais Putin anazingatia kwa umakini suala zima la mazungumzo ya amani na Ukraine.
Soma pia: Lammy kuwa mwenyeji wa Weimar+ kwa mazungumzo juu ya Ukraine
Hayo yakiendelea, Urusi ilifanya mashambulizi makubwa ya droni zaidi ya 100 nchini Ukraine, kama ishara ya kutupilia mbali miito ya Ukraine na washirika wake wa Magharibi waliokuwa wamependekeza usitishwaji mapigano kwa siku 30 kuanzia leo Jumatatu. Mashambulizi ya Urusi katika mkoa wa kaskazini mwa Ukraine wa Sumy yamesababisha pia vifo vya watu watatu huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.
Urusi na Ukraine zote zinajaribu kumuonyesha Rais wa Marekani Donald Trump kwamba wanafanyia kazi pendekezo lake la kufikia amani ya haraka na kudumu nchini Ukraine, lakini wakati huohuo nchi hizo mbili hasimu zimekuwa zikijaribu pia kutupiana lawama ili kutwishana dhima ya kuvuruga juhudi hizo.
(Vyanzo: Mashirika)