Viongozi wa Ulaya wanakutana kwa dharura Paris
17 Februari 2025Ametoa kauli hiyo Jumatatu 17.02.2025 muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano huo unaolenga kuyajadili mabadiliko ya sera za Marekani kuhusu kuumaliza mzozo Ukraine.
Muda mfupi baada ya kuwasili Paris, Von der Leyen amesema ni kweli wanajadili usalama wa Ukraine lakini pia suala hilo la mabadiliko ya kiusalama linauhusu pia Umoja wa Ulaya.
Kupitia Ukurasa wake wa X von der Leyen ameeleza kwamba Ulaya inahitaji mawazo ya haraka juu ya jambo hilo na kuongeza ulinzi.
Mkutano huo wa dharura wa viongozi wa Ulaya mjini Paris, unafanyika baada ya mkutano wa usalama wa mjini Munich uliokwisha Jumapili kushindwa kukamilika huku ukiwa umegubikwa na hali ya sintofahamu hasa kutokana na msimamo wa Marekani juu ya namna ya kuvimaliza vita vya Ukraine.
Soma zaidi: Mkutano wa dharura waitishwa Paris baada ya tofauti za wazi za Ulaya na Marekani
Rais wa Marekani Donald Trump aliitenga Ukraine na washirika wake wa Ulaya wiki iliyopita alipompigia Rais wa Urusi Vladmir Putin ili kuanza mazungumzo ya kuumaliza mzozo huo
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Stammer wakati akielekea kwenye mkutano huo wa dharura ametoa wito kuwa, makubaliano yoyote kuhusu kuumaliza mzozo wa Ukraine yanapaswa kuwa ya haki na ya kudumu. Ameongeza kuwa majibu yenye uhalisia na ya uhakika yanahitajika ili kuhakikisha makubaliano yoyote ya kusitisha vita yanadumu.
Mkutano huo unaendelea wakati kukiwa na mjadala mwingine kuhusu Ulaya kupeleka wanajeshi Ukraine. Mjadala huo umeibuka baada ya Uingereza kusema kuwa iko tayari kwa hatua ya aina hiyo.
Ujerumani kwa upande wake imesema ni mapema mno kuchukua hatua ya aina hiyo. Nchi nyingine zikiwemo Denmark, Slovakia na Uhispania pia zimesema kwa sasa ni mapema kuzungumzia suala la kupeleka vikosi nchini humo.
Kuhusu suala hilohilo, waziri Mkuu wa Poland Donald Tusk amesema, "Ninajua kuna tetesi nyingi na taarifa za kubahatisha bahatisha ikiwa tutajadili kwenye mkutano huu wa Paris kuhusu nani, wakati gani na kama tuko tayari kupeleka wanajeshi. Ukraine. Kwa upande wa Poland, tutaiunga mkono Ukraine kama ilivyo hadi sasa, kuratibu, kifedha na kadri ya uwezo wetu kutoa misaada ya kiutu na kijeshi lakini Hatuna mpango wa kupeleka wanajeshi wa Poland Ukraine."
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban ambaye ni mshirika wa karibu wa Donald Trump na Vladimir Putin amesema mkutano wa dharura wa viongozi wa Ulaya ni unaofanyika Paris ni juhudi za kuzuia amani ya Ukraine
Wakati huo huo, Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov amesema haoni sababu ya Ulaya kuwa sehemu ya mazungumzo ya kusitisha vita Ukraine na badala yake Lavrov ameutuhumu umoja huo kuwa unataka vita nchini Ukraine viendelee.
Ameyatoa maoni hayo kabla ya kuelekea Saudi Arabia kukutana na maafisa wa Marekani wakati viongozi wa Ulaya wakifanya mkutano wa dharura kuhusu Ukraine.