Viongozi EU wakusanyika Paris kujadili hatma ya Ukraine
17 Februari 2025Viongozi hao wanaketi wakati kukiwa na kiwingu cha mashaka kwamba kanda hiyo inaweza kutengwa kwenye mazungumzo ya kutafuta amani ya Ukraine.
Ikulu ya Ufaransa, Elysee, imesema wenyeji wa mkutano huo, Rais Emmanuel Macron anataka Ulaya itafute msimamo wa pamoja kuhusu amani ya Ukraine na ichukue jukumu kubwa zaidi la usalama wake yenyewe baada ya miongo mingi ya kuitegemea Marekani.
Soma pia: Viongozi wa Ulaya wakutana kwa dharura kujadili usalama wa Ukraine na Ulaya
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema baada ya kuwasili mjini Paris, kuwa Ulaya inapaswa kubadili mtazamo wake juu ya suala la usalama ikiwa ni pamoja na kuongeza matumizi kwenye sekta ya ulinzi.
Mbali ya wakuu wa Umoja wa Ulaya mkutano huo utahudhuriwa pia na viongozi wa Ujerumani, Uingereza, Italia, Poland, Uhispania, Denmark na Uholanzi pamoja Katibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO.