Viongozi wa Ulaya wakubaliana kuhusu amani ya Ukraine
3 Machi 2025Mazungumzo hayo, ambayo yaliwaleta Pamoja washirika 18, yalijiri siku mbili tu baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kumshambulia Volodymyr Zelensky wa Ukraine mbele ya waandishi Habari katika Ikulu ya White House.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmeramesema Uingereza, Ufaransa na "wengine" watashirikiana na Ukraine kuhusu mpango wa kusitisha mapigano, ambao kisha watauwasilisha kwa Washington.
Malumbano ya Trump na Zelensky pia yalizusha maswali mapya kuhusu dhamira ya Marekani kwa Jumuiya ya Kujihami ya NATO. Starmer amesema Ulaya imejikuta "kwenye njia panda katika historia. Huu sio wakati wa mazungumzo zaidi – ni wakati wa kuchukua hatua. Ni wakati wa kujitokeza na kuongoza na kuunga mkono mpango mpya wa amani ya haki na ya kudumu.” Bila hakikisho la kuhusika kwa Marekani, "Ulaya lazima ifanye kazi kubwa,” amesema Starmer.
Ufaransa na Uingereza zependekeza makubaliano ya amani kwa mwezi mmoja Ukraine
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, akiwa njiani kurejea nyumbani kutoka kwenye mkutano huo wa kilele, amesema katika mahojiano ya gazeti kuwa Ufaransa na Uingereza zinataka kupendekeza makubaliano ya muda ya amani ya mwezi mmoja.
Ameliambia gazeti la Ufaransa Le Figaro, kuwa yeye na Starmer wanalifanyia kazi pendekezo hilo la amani nchini Ukraine litakalohusu usitishaji mapigano, "angani, baharini, na kwenye miundo mbinu ya nishati.”
Zelensky anaamini uhusiano na Trump unaweza kuokolewa
Zelensky alikaribishwa na kukumbatiwa na viongozi wengi wa ulimwengu kwenye mkutano huo wa kilele. Alisema anaamini kuwa angeweza kuokoa uhusiano wake na Rais wa Marekani Donald Trump baada ya kuzozana kwao hadharani katika Ofisi ya Oval. Zelenskyy alisema, "Muundo wa kile kilichotokea, sidhani kama kilileta kitu chanya au cha ziada kwetu kama washirika."
Zelenskyy alipuuzilia mbali wazo kwamba Marekani itaacha kuunga mkono Ukraine kwa sababu kama "viongozi wa ulimwengu uliostaarabika" hawatataka kumsaidia Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Lakini kiongozi huyo wa Ukraine alisema bado yuko tayari kukabiliana na changamoto zozote zinazoweza kutokea. "Tuko tayari kusaini mkataba wa madini na ninaamini Marekani itakuwa tayari pia," aliongeza.
Maafisa wa Urusi wakejeli mkutano wa London kuhusu Ukraine
Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev ameuita mkutano huo wa kilele wa London "muonekano wa aibu”, kwenye ujumbe alioandika kwenye mtandao wa kijamii wa X. Medvedev, ambaye sasa ni naibu mkuu wa Baraza la Usalama la Urusi, aliupuuzilia mbali mkutano huo akisema ni mapatano….ya kuapa utiifu kwa Manazi wasiokuwa na maana yoyote huko Kyiv.”
Mbunge wa Urusi Konstantin Kosachev alikejeli matokeo ya mazungumzo hayo ya Ukraine mjini London kama "jaribio la kukata tamaa la kupitisha kama mafanikio, kushindwa kwa sera ya miaka 10 ya kuichochea Ukraine kuelekea Urusi na Uingereza hiyo hiyo na, hadi hivi karibuni, Marekani."
"Ulaya haina mpango," aliandika Kosachev, mkuu wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Baraza la Shirikisho – baraza la juu la bunge la Urusi, kwenye Telegram.
Afp, ap, reuters, dpa