Mzozo wa Ukraine: Viongozi wa Ulaya wafanya ziara Marekani
28 Februari 2025Baada ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, jana ilikuwa zamu ya Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ambaye amesema mkataba wa amani kuhusu mzozo wa Ukraine unapaswa kuwa wa kudumu:
"Mkataba huo lazima uwe wa kudumu. Lazima liwe jambo la kudumu. Na ili kulifanikisha hilo, kuna haja ya kuwa na nia ya dhati kutoka kwa Putin kwamba hawezi kukiuka mpango huo. Na ndio maana nimekuwa nikisema mara kadhaa kuwa, nadhani nchi za Ulaya, ikiwemo Uingereza, zinatakiwa kushirikishwa kikamilifu katika mchakato huo."
Siku ya Ijumaa, Trump atampokea rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ambapo miongoni mwa mambo mengine kuhusu vita, watajadili namna ya kuiwezesha Marekani kupata madini adimu ya Ukraine.
Soma pia: Trump amkaribisha Starmer bila ahadi ya usalama kwa Ulaya
Baadaye siku ya Jumapili, Waziri Mkuu huyo wa Uingereza ameandaa mkutano wa kilele na viongozi kadhaa wa Ulaya kutoka Ufaransa, Ujerumani, Denmark, Italia, Uholanzi, Norway, Poland, Uhispania, Finland, Sweden, Jamhuri ya Czech, Romania pamoja na Uturuki ili kuelezea aliyoyajadili na Trump na kujadili kuhusu usalama wa Ulaya. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya kujihami ya NATO Mark Rutte na mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na rais wa Baraza Kuu la umoja huo Antonio Costa wamealikwa kwenye mkutano huo wa kilele mjini London.
Urusi na Ukraine zaendelea kushambuliana
Mashambulizi ya makombora na droni yamesababisha vifo vya watu watatu katika eneo linalokaliwa na Urusi katika mkoa wa Kherson. Shirika la habari la Urusi RIA limesema watu hao ni mwanamke na mtoto mmoja ambao waliuawa baada ya gari la wagonjwa kushambuliwa katika kijiji cha Mala Lepetykha huku mtu mwengine akiuawa katika kijiji cha Oleshky.
Kwa upande wake, Jeshi la Ukraine limesema limedungua droni zipatazo 107 kati ya 208 zilizorushwa na Urusi usiku wa kuamkia leo huku zingine 97 zikishindwa kufikia shabaha yao kutokana na ufanisi wa mifumo ya ulinzi wa anga.
Aidha, idara ya usalama ya Urusi FSB imefahamisha leo kuwa imezuia jaribio la Ukraine la kumuua kiongozi mkuu wa kanisa la Othodoksi la Urusi aliyefahamika kwa jina la Tikhon Shevkunov, 66, ambaye pia ni mjumbe wa baraza la ushauri la rais Vladimir Putin anayehusika na masuala ya utamaduni na sanaa.
(Vyanzo: Mashirika)