Viongozi wa EU kujadili mpango wa Trump kuhusu Ukraine
17 Februari 2025Mkutano huo uliotishwa na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa utawaleta pamoja viongozi wa Ujerumani, Uingerzea, Italia, Poland, Uhispania, Denmark na Uholanzi pamoja na viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya NATO.
Unafanyika katika wakati wasiwasi ni mkubwa kwamba bara hilo huenda litapigwa kumbo kwenye meza ya mazungumzo.
Soma pia:Trump atangaza kukutana na Putin siku za usoni
Dhima ya mkutano huo ni kutafuta mkakati wa pamoja kuelekea utawala mpya mjini Washington hasa kuhusu masuala ambayo Ulaya haitoyakubali kwenye mchakato wa kusaka amani na kumaliza vita vya Ukraine.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Ufaransa, Elysee, imesema Rais Macron analenga kuutumia mkutano huo kujadili hali nchini Ukraine na changamoto za usalama zinazolikabili sasa bara la Ulaya.